December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TRA wajipanga kukusanya zaidi ya Tril. 30

Na Allan Kitwe, TimesMajira Online, Tabora

MAMLAKA ya Mapato nchini (TRA) wanatarajia kukusanya zaidi ya sh trilioni 30.4 katika mwaka wa fedha 2024/25 ikiwa ni ongezeko la kiasi cha sh trilioni 2.1 za makusanyo waliyopata katika mwaka wa fedha uliopita 2023/24.

Hayo yamebainishwa jana na Meneja wa Mamlaka hiyo Mkoani hapa Fedrick Kanyilili alipokuwa akifungua mafunzo ya elimu ya mabadiliko ya sheria mpya ya ulipaji kodi kwa wakandarasi wa Mkoa huo yaliyofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Grand Penta mjini hapa.

Amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2023/24 Mamlaka hiyo ilikusanya jumla ya sh trilioni 28.30 na mkakati wa mwaka huu ni kuvuka malengo ya kiasi hicho kwa kukusanya sh trilioni 2.1 zaidi sawa na ongezeko la asilimia 7.42.

Amebainisha kuwa ukusanyaji huo ni muhimu sana kwa maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla kwa kuwa fedha hizo zitasaidia kuchochea kasi ya maendeleo ya wananchi ikiwemo kuboreshwa miundombinu ya huduma za kijamii katika Mikoa yote.

‘Naomba wakandarasi wote muwe wazalendo wa kweli kwa kulipa kodi kwa wakati bila kushurutishwa pia kuendelea kujenga heshima yenu kwa wadau mnao wahudumia ikiwemo kuendelea kuaminiwa na serikali’, amesema.

Kanyilili amesisitiza matumizi ya mashine za EFD kwa wakandarasi na wafanyabiashara wote punde wanapotoa huduma kwa wananchi na kuwataka kuacha kutumia risiti za mkono.

Aidha amewataka wafanyabiashara wote kulipa kodi kwa wakati ili kuepuka kupigwa faini huku akiwakumbusha kuwa Ofisi ya Mamlaka hiyo ipo tayari kuwahudumia wakati wote.

Amebainisha kuwa siku ya Alhamisi wanatoa huduma ya kupokea taarifa, maoni, changamoto, maswali na jambo lolote linalohusiana na kodi kutoka kwa wakandarasi, wafanyabiashara na wadu wengineo.

‘TRA ipo kwa ajili ya kuwahudumia wadau wote, ikiwemo kuwapa elimu sahihi ya ulipaji kodi, haipo kwa ajili ya kuwagandamiza, kuwapiga faini au kuchochea migogoro, kinachotakiwa ni ushirikiano baina ya Mamlaka na Wadau, amesema.

Mwenyekiti wa Wakandarasi wa Mkoa wa Tabora Frank Mgonja amewaasa wenzake kupokea mafunzo hayo na kufanyia kazi maelekezo yote ili kuleta chanya tija katika shughuli zao na kuondokana na fikra potovu kuwa TRA ni adui yao.

Ameshauri Mamlaka hiyo kwa kushirikiana na Uongozi wa Wakandarasi Mkoani hapa kuwatambua wanachama walio hai badala ya kuwa na orodha ndefu isiyokuwa na uhalisia.