Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Korogwe
MAMLAKA ya Mapato Tanzania(TRA)Mkoa wa Tanga imewataka Watanzania kuonesha uzalendo kwa kufichua watu wanaofanya biashara ya magendo,kwani biashara hiyo haipotezi mapato ya Serikali tu,bali pia inaua biashara za wengine wanaofanya biashara kwa kufuata sheria za nchi.
Na katika kuweza kuwafanya wananchi waweze kuwabaini watu hao na kutoa taarifa kwa TRA ama vyombo vya ulinzi na usalama, TRA inatoa motisha kwa mtu atakaeweza kutoa taarifa za kukamatwa mzigo wa magendo, na atazawadia fedha asilimia 20 ya thamani ya mzigo huo.
Hayo yamesemwa Septemba 18, 2024 na watoa mada kwenye mafunzo ya siku moja yaliyotolewa na TRA kwa wafanyabiashara wa Wilaya ya Korogwe, na kufanyika mjini Korogwe, ikiwa ni muendelezo wa kutoa elimu kwa wafanyabiashara hao juu ya mienendo ya ulipaji kodi nchini.
“Watanzania wanatakiwa kuonesha uzalendo kwa kuwafichua watu wanaofanya biashara za magendo. Watu hao wanarudisha nyuma maendeleo ya nchi sababu wanapoteza mapato ya Serikali,lakini pia wanaharibu biashara za wengine,Mfano ndoo ya mafuta ya lita 20 ni sh. 85,000, lakini yeye anaiuza kwa sh. 40,000, na wewe wala hustuki, bali unanunua tu,huko ni kuharibu biashara ya watu wengine.
“Kwa kuliona hilo, TRA imeweka motisha kwa watu watakaoweza kushirikiana na TRA ili kuwabaini wanaofanya biashara ya magendo,hivyo kila mtu atakaeweza au kuwezesha TRA kukamata mali ya magendo, atapewa fedha asilimia 20 ya mali ya magendo iliyokamatwa”amesema Jesca Kapori, Afisa Forodha Mkoa wa Tanga.
Naye Afisa wa Kodi Wilaya ya Korogwe Innocent Mushi amesema wameweka mikakati ya kupambana na watu wanaofanya biashara ya magendo na wanajua Korogwe ni sehemu ya watu wanaotumia biashara ya magendo, na njia wanazopita wanazijua, kuanzia bandari bubu za Wilaya ya Pangani, njia ya mkato ya kutoka Pangani hadi Muheza, kutoka Muheza hadi Kijiji cha Maguzoni.
Amesema baada ya hapo wanaingia Shamba Kapori hadi Mnyuzi, halafu wanakwenda kutokea Old Korogwe na kuingia Korogwe mjini, na hiyo ni kwa ajili ya kukwepa Kituo cha Ukaguzi cha TRA Segera.
“Tunajua, Korogwe wapo watu wanafanya biashara ya magendo lakini na sisi tumeweka watu wetu ambao ni Informer (watoa taarifa) na tunajukumu wakitoa mizigo Pangani wanapitia wapi,wakitoka Pangani wanapitia njia short cut ya Muheza hadi Maguzoni, halafu wanaingia ndani (Mnyuzi) ili kuja kutokea Korogwe na hiyo ni kuwa wanakwepa ukaguzi pale Segera,”amesema Mushi.
Mmoja wa wafanyabiashara Edistariki Marandu amewataka maofisa wa TRA kuweka mikakati ya kupambana na wafanyabiashara wanaofanya biashara ya magendo, kwani watu hao wanafifisha biashara za wengine wanaofanya kwa kufuata Sheria, kanuni na taratibu za nchi.
Akifungua mafunzo hayo, Meneja wa TRA Wilaya ya Korogwe Evason Lushaka amesema mafunzo hayo ni kwa ajili ya kujenga uelewa, elimu na kubwa zaidi kuweka maelewano mazuri pamoja na na walipa kodi na amesisitiza kwamba watumie majukwaa hayo kuweza kukutana na kubadilishana mawazo kwani kukutana na mtu mmoja mmoja inaweza kuwa vigumu, lakini kwa kuwepo watoa mada, changamoto nyingi zinaweza kupatiwa ufumbuzi.
“Naamini kupitia mafunzo haya, tunapotengeneza uelewa inaweza isiwe lazima kunifikia moja kwa moja na hawa ni wataalamu wametoka mkoani na wamefika hapa wilayani kwa ajili ya kutusaidia kupata uelewa lakini pia, panapotokea mabadiliko ya sheria, mada zetu kadha wa kadha zinakuwa zimebadilika, sasa unaweza kuweka na ile dhana ya mazoea halafu katika utekelezaji mtu akawa hafahamu kuwa kuna mabadiliko kuwa yamejitokeza.
“Na ukielewa kuwa kwa sasa changamoto kubwa ya watu, kufuatilia yale mambo ya umuhimu unakuta ni ngumu sana, hivyo kupitia mafunzo kama haya tunapata wasaa wa kupata elimu mbalimbali, lakini pia kupata changamoto ambazo huenda hukuweza kunifikia ofisini, lakini kwa kuwa nipo hapa, naweza kuzijibu,”amesema Lushaka.
Afisa Mkuu wa Elimu kwa Mlipa Kodi Mkoa wa Tanga.”
More Stories
Bodaboda wamchangia Rais Samia Mil 1 ya fomu ya Urais
HAYA HAPA MATOKEO YOTE FORM II NA DARASA LA IV
Ufaulu waongezeka matokeo ya Darasa la Nne na Kidato cha Pili