January 15, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TPDC kuongeza kasi ya upatikanaji wa Gesi nchini

Na Penina Malundo,timesmajira, Online

AFISA Uhusiano wa Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC), Fransis Lupokela amesema TPDC inaendelea kuongeza kasi ya upatikanaji wa gesi asilia katika vyanzo mbalimbali ambapo hadi sasa watafiti wapo kazini kutafuta gesi na mafuta nchini.

Pia amesema tayari kuna viwanda nane vinavyotumia gesi asilia, nyumba 1500 na Hoteli, Taasisi mbalimbali za serikali ambazo ni Gereza la Mtwara na la Keko pamoja na shule nne na Magari 1400 zinazotumia nishati ya Gesi Asilia.

Akiongea na waandishi wa habari jana wakati wa maonesho ya Kimataifa ya kibiashara ya 46 katika Viwanja vya J.K. Nyerere maarufu kama Sabasaba jijini Dar es Salaam leo, amesema TPDC imefanikiwa kugundua gesi katika maeneo mbalimbali nchini na kutekeleza miradi mbalimbali kuhakikisha gesi asilia inapatikana nchini.

Baadhi ya wananchi wakiofika katika banda la TPDC wakipokea maelezo.

Amesema miongoni mwa kazi zinazofanywa na shirika ni pamoja na kufanya shughuli za utafiti wa mafuta na Gesi katika mkondo wa Juu wa Kati na wachini.

Lupokela amesema katika Mkondo wa juu shirika linamiradi ya kimkakati ya ambayo ni Eyasi ni mradi ambao wanatafuta mafuta na gesi katika ziwa Eyasi, linalogusa mikoa ya Singida, Arusha, Tabora na Simiyu.

Lupokela amesema katika Mradi wa Mnazi Bay Kaskazini (North) wanaendelea kufanya tafiti za kugundua gesi pamoja na mradi wa Songosongo (west) Magharibi

Amesema nchi mpaka sasa inamiundombinu Mitatu ya gesi asilia ambayo ni Songas, NMP ambao unaishia Mtwara na Miundombinu ya taifa ya gesi asilia (NGI), ambalo ni bomba kubwa la gesi asilia ambalo linasaidia kuzalisha umeme kwa asilimia 62 ambao upo kwenye gridi ya Taifa unazalishwa kutokana na gesi asilia.

“Katika maonesho ya sabasaba tunaonesha wananchi juu ya matumizi ya gesi asilia na kuonesha namna gani viwanda vinatumia gesi asilia pamoja na Mahoteli.” Amesema Lupokela

Katika kuhakikisha gesi asilia inapatikana majumbani amesema kuwa shirika la TPDC linaendelea kufanya tafiti za kuongeza upatikanaji wa gesi tayari serikali imeruhusu Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kushirikiana na TPDC wanafadhili ili kuwezesha ujenzi wa miundombinu ya kusambaza gesi.

Ili kuhakikisha kwamba gesi asilia inafika maeneo ya mikoani tayari wamejipanga kusambaza kwa njia tatu ambazo zinaweza kufikisha gesi hiyo kwa njia ya mabomba na usindikaji wa gesi katika maeneo husika.