January 7, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TPB kuendelea kuthamini wastaafu

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

OFISA Mtendaji Mkuu wa Benki ya TPB, Sabasaba Moshingi ameahidi kuendelea kutoa huduma bora na mikopo kwa wastaafu hapa nchini.

Katika bara la Afrika, Tanzania kupitia benki hiyo ilikuwa nchi ya pili kutoa mikopo kwa wastaafu ikiwa kama njia mojawapo ya kutambua mchango wa wazee hao ambao kwa sasa wamestaafu.

Akizungumza katika Tawi la Metropolitan alipotembelea kwa ajili ya maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Mteja, Moshingi amesema moja ya mambo muhimu yaliyofanywa na benki yake ni kutoa mikopo kwa wastaafu, jambo ambalo halikufikiriwa popote hapa nchini.

Amesema kuwa, waliamini kuwa mikopo hiyo, itawawezesha kuendelea vizuri na maisha yao na kweli imekuwa na faida, kwani wamepata shuhuda mbalimbali kutoka kwa wateja wao ambao wamepatiwa mikopo.

“Niwashukuru sana wastaafu ambao siku zote wameendelea kupata mikopo kutoka kwetu na tunaahidi kuendelea kuwa nao pamoja, kwani tupo kwa ajili yao kwa kuwa tunaamini sisi ni timu moja na tupo kutimiza ndoto zetu,” amesema Moshingi.

Akizungumzia juu ya ajira kwa vijana, Moshingi amesema, wanatambua kuwa bado kuna changamoto kubwa ya ajira, kwani vijana wanaomaliza vyuo ni wengi ikilinganishwa na ajira zilizopo na ndiyo maana wameajiri vijana wengi.

“Wakati tunaanza miaka nane iliyopita, tulikuwa na wafanyakazi 400 lakini kwa sisi kama taasisi tumekuwa na mabadiliko makubwa sana, kwani tuna wafanyakazi zaidi ya 1,200 hivyo ajira mpya tulizotoa ni zaidi ya 700 kwa vijana wetu wa Kitanzania,” amesema Moshingi.

Kwa vijana ambao wanajiajiri, Moshingi amesema, kuna aina mbalimbali za mikopo kuanzia ngazi ya vikundi na mitaji kwa wenye biashara zilizokuwa na wapo tayari kuendelea kuwasaidia kukuza mahitaji yao.

Akielezea huduma zinazotolewa na TPB, mmoja wa wateja wa benki hiyo ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bima la Taifa, Dkt. Elirehema Doriye amesema, kwa muda mrefu wamekuwa wakifanya kazi na benki hiyo na mara zote, wamekuwa wakipatiwa huduma kwa uhakika ikiwemo kwa njia ya mtandao.

Amesema kwa sasa kwao, TPB ni kama daraja na kuhakikisha kuwa wanatoa huduma nzuri kwa wateja wao kutokana na huduma bora wanazopata, kwani kumekuwa na wafanyakazi maalumu kwa kuhudumia wateja wakubwa na wadogo.

Meneja wa tawi la Metropolitan, Lilian Mboya amesema, katika maadhimisho ya Wiki ya Mteja wanaendelea kupokea maoni mbalimbali kutoka kwa wateja wao, kwani kuna maswali mengi ya kibiashara kuhusiana na huduma za kibenki wanahitaji kuzijua.

“Ili kutoa huduma bora kwa wateja ni lazima usikilize maoni yao, hivyo si katika wiki hii tu bali kila siku tutaendelea kuwapa kile wanachokihitaji kwa wakati na tumejipanga kuwapa kile kilicho bora zaidi ya awali,”.