April 7, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TMDA yajivunia kuanzisha mfumo thabiti wa udhibiti wa vifaa tiba na vitendanishi

Na Penina Malundo, TimesMajira Online

MKURUGENZI wa Uendeshaji huduma wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba(TMDA)Chrispin Severe amesema miongoni mwa mafanikio makubwa ya TMDA inayojivunia ni pamoja na kuwa taasisi ya kwanza barani Afrika kuanzisha mfumo thabiti wa udhibiti wa vifaa tiba na vitendanishi.

Ameyasema hayo wakati wa Kikao kazi kati ya TMDA na Waandishi wa habari juu ya Muundo,Majukumu na Mafanikio ya TMDA,amesema TMDA pia imeanzisha na kutumia mifumo ya  kieletroniki kwa ajili ya huduma mbalimbali ikiwemo Import Online System, Clinical Trials Registry, RIMS, LIMS, SQRT,ikiwa na lengo la kusogeza huduma kwa ukaribu zaidi.

Amesema tayari wameweza kujenga jengo la Ofisi na maabara kwa mikoa ya  Dar es salaam, Mwanza na Dodoma.”mafanikio haya yanaonesha kwa kiasi gani tumejipanga katika kusogeza huduma kwa ukaribu zaidi kwa  wananchi kwa kufungua Ofisi za Kanda zinazofanya kazi kwa ufanisi na kujenga jengo la Ofisi  na maabara katika mikoa mitatu.

”Pia TMDA tumefanikiwa kupata Hati Safi za Ukaguzi (Clean Audit Reports) kupitia kaguzi za CAG tangu kuanzishwa kwa taasisi huku tukiendelea kudhibiti uingizaji na utoaji nje ya nchi wa bidhaa ikiwa ni pamoja na dawa tiba zenye madhara ya kulevya,”Amesema.

Aidha amesema pia  wamekuwa wakidhibiti matangazo ya biashara ya bidhaa mbalimbali ambazo hazijafata kanuni wala sheria za mamlaka hiyo na Kuelimisha jamii kuhusu ubora, usalama na matumizi sahihi ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi.

Akitaja changamoto ambazo TMDA wanakabiliana nazo,Severe amesema miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na matangazo ya bidhaa za dawa, vifaa tiba na vitendanishi kwenye baadhi ya vyombo vya Habari na mitandao ya kijamii bila kibali cha TMDA.”Utakuta watu wanatoa matangazo ya bidhaa zao za dawa katika vyombo vya habari bila kuwa na kibali TMDA hii ni kosa wanapaswa kuja katika ofisi zetu na kupewa kibali maalum cha utoaji wa matangazo yao kulingana na sheria na kanuni zetu.

”Pia matumizi ya mitandao nayo imekuwa ni changamoto katika  kupotosha umma juu ya bidhaa zinazodhibitiwa na kuleta ugumu katika kuwapata wahusika (cyber crime through excessive and unethical use of social media),”amesema Severe.

Amesema bado kuna uelewa mdogo wa wadau hususan wananchi juu ya mahitaji ya sheria, kutambua bidhaa duni na bandia na wajibu wao katika kulinda afya ya jamii kwa kutoa taarifa za usalama na ubora bidhaa.