January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TMA:Wanahabari toeni taarifa ya hali ya hewa kwa usahihi na wakati

Na Penina Malundo,Dar es Salaam

KAIMU Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA), ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi,Dkt Ladislaus Chang’a amewasisitiza waandishi wa habari kuendelea kusambaza taarifa za hali ya hewa kwa usahihi na kwa wakati zinazotolewa na TMA ili kusaidia jamii,taasisi za maafa pamoja na serikali kujiweka tayari kukabiliana na madhara ya hali ya hewa yanayoweza kutokea.

Rai imetolewa leo mkoani Pwani wakati wa warsha ya mafunzo kwa wanahabari kuhusu Msimu wa Mvua za Vuli 2023,Kaimu Mkurugenzi wa TMA,Chang’a amesema mamlaka hiyo inajitahidi kutoa taarifa zake mapema na kwa wakati ili ziweze kuwafikia wananchi na sekta husika mapema kwa ajili ya kuwawezesh kuchukua hatua stahiki mapema.

Amesema kuna umuhimu mkubwa wa matumizi ya hali ya hewa kwa jamii katika shughuli zao za kila siku hivyo ni vyema wanahabari kutoa habari sahihi kwa wananchi.”Warsha hii ni mwendelezo wa juhudi za Mamlaka katika kuhakikisha taarifa zake hasa za utabiri wa hali ya hewa zinawafikia walengwa ikiwemo jamii kwa uhakika na usahihi zaidi,”amesema na kuongeza

”Taarifa za hali ya hewa zikiifikia jamii kwa haraka ,uhakika na usahihi itasaidia jamii kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa na kusaidia mamlaka mamlaka zinazohusika kupanga mipango ya kukabiliana na majanga yatokanayo na hali mbaya ya hewa,upatikanaji wa chakula na lishe bora pamoja na afya kwa ustawi wa jamii,”amesema Chang’a.

Amesema msimu unaokuja wa Oktoba hadi Disemba 2023 kwa kiasi kikubwa unaweza kuathiriwa na hali ya El Nino ambapo moja ya athari za El Nino kwa nchi ya Tanzania ni kupongezeka kwa viwango vya mvua na joto kwa baadhi ya maeneo nchini.

Dkt. Chang’a ametaja maeneo hayo ni yale yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka,El Nino ni hali ya kuongezeka kwa jotola uso wa bahari wa eneo la kitropiki la kati ya bahari ya Pasifiki.