December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TMA:Hakuna tishio la Kimbunga “IALY”tena

Na Penina Malundo, Timesmajira

MAMLAKA ya Hali ya hewa nchini(TMA),imesema kwa sasa hakuna tena tishio la kimbunga “IALY” katika nchi ya Tanzania kwani kimbunga  hicho kimepoteza kabisa nguvu yake, kikiwa kaskazini mashariki mwa pwani ya Kenya. 

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana jijini Dar es Salaam na Mamlaka hiyo imesema mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa unaonesha kuwa katika kipindi cha saa 6 zilizopita, Kimbunga “IALY” kimepoteza nguvu zake.

Ilisema wakati kikipita karibu na pwani ya nchi ya Tanzania kati ya jana na leo kimeweza kusababisha vipindi vya mvua, upepo mkali na mawimbi makubwa katika maeneo ya pwani ya nchi yetu kama ilivyotabiriwa awali.

”Ikumbukwe kuwa, japo tunaelekea mwishoni mwa msimu wa Masika, 2024, tunakaribia kuanza kwa msimu wa Kipupwe, na kwasababu hiyo, vipindi vya upepo wa Kusi baharini vinaweza kuanza kujitokeza na kuambatana na mawimbi makubwa kwa baadhi ya nyakati,”imesema taarifa hiyo na kuongeza

”Mamlaka ya TMA inatoa ushauri wananchi na watumiaji wa bahari wanashauriwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na maelekezo na miongozo inayotolewa na mamlaka husika,”Imesema taarifa hiyo.

Aidha taarifa hiyo imesema kuwa taarifa hii ni hitimisho la  mfululizo wa taarifa za kilichokuwa Kimbunga “IALY” zilizokuwa zikitolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) tangu mei 17,2024.