Na Penina Malundo
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema mvua za msimu wa Vuli zinazotarajia kuanza kunyesha Oktoba hadi Disemba mwaka huu zinatarajia kuwa Juu ya wastani hadi wastani.
Mvua hizo zinatarajia kuwa na uwepo wa El-Niño nchini katika msimu huo wa mvua za vuli.
Hayo yalisemwa leo jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC) wakati wa mkutano na vyombo vya habari kuhusiana na mwelekeo wa msimu wa mvua za Vuli (Oktoba hadi Disemba 2023), amesema kutokana na uwepo wa El-Niño, vipindi vifupi vya mvua vinatarajiwa kwa mwezi Septemba, 2023 katika baadhi ya maeneo nchini, hata hivyo, mvua za Vuli, 2023 zinatarajiwa kuanza rasmi mwezi Oktoba, 2023 katika maeneo mengi.
Amesema mvua za Juu ya Wastani hadi Wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, kusini mwa mkoa wa Simiyu, kaskazini mwa mkoa wa Kigoma, Dar es Salaam, Tanga, Pwani (ikiwemo visiwa vya Mafia), kaskazini mwa mkoa wa Morogoro na pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba katika msimu wa mvua za Vuli, 2023.
Ametaja maeneo mengine ya mikoa ya Mara, kaskazini mwa mkoa wa Simiyu, Arusha, Manyara na Kilimanjaro yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.
“Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Septemba, 2023 katika maeneo ya magharibi mwa Ziwa Victoria na kusambaa katika maeneo mengine mwezi Oktoba, 2023. Kwa kawaida mvua za Vuli huisha mwezi Disemba, hata hivyo msimu huu mvua za nje ya msimu zinatarajiwa kuendelea mwezi Januari, 2024. Ongezeko la mvua linatarajiwa mwezi Disemba, 2023”. Amesema Dkt. Chang’a.
Dkt. Chang’a ametoa wito kwa wananchi kufuatilia taarifa za utabiri wa saa24, siku 10, mwezi natahadhari zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ikizingatiwa kuwa mwelekeo wa mvua uliotolewa ni kipindi cha msimu wa miezi mitatu, hivyo viashairia vinavyochangia mwenendo wa mifumo ya mvua na mabadaliko ya muda mfupi utazingatiwa katika uchambuzi wa utabiri wa muda wa kati na mfupi.
Dkt. Chang’a amesema, TMA itaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa mirejesho ya mwelekeo wa mvua nchini kadri inavyohitajika. Aidha, wadau wanashauriwa kuwasiliana na Mamlaka ili kupata taarifa mahsusi za utabiri wa msimu ili kukidhi mahitaji maalum katika sekta zao.
Msimu wa Mvua za Vuli ni mahususi kwa maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki (Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro), pwani ya kaskazini (kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, mikoa ya Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba), ukanda wa Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara) pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato