November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TMA :Mvua za vuli zinatarajia kuanza mwishoni mwa Septemba 2024

Na Penina Malundo,Timesmajira

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Nchini(TMA),imesema kuwa mvua za msimu wa vuli kwa Kipindi cha Oktoba hadi Disemba 2024,zinatarajia kuanza wiki ya nne ya mwezi Septemba 2024 katika maeneo ya magharibi ya kanda ya Ziwa Victoria na kusambaa katika maeneo mengine kwa mwezi Oktoba 2024.

Mvua hizo zinatarajia kunyesha chini ya wastani hadi wastani,huku vipindi vya joto kali kuliko kawaida vinatarajia kujitokeza.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati akitoa mwelekeo wa mvua za msimu wa vuli Oktoba hadi Disemba 2024 kwa waandishi wa habari,Kaimu Mkurugenzi wa TMA ,Dkt.Ladislaus Chang’a amesema mvua hizo za vuli na mahususi kwa maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki ikiwemo (Arusha,Manyara na Kilimanjaro,Mikoa ya Pwani ya Kaskazini ikiwemo mkoa wa Morogoro,Pwani,Dar es Salaam,Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.

Amesema mikoa mingine ni pamoja na ukanda wa Ziwa Viktoria ikiwemo mkoa wa Kagera,Geita,Mwanza,Shinyanga,Simiyu,Mara pamoja na Kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.
”Mvua hizi zinatarajiwa kuishi katika wiki ya nne ya mwezi Disemba 2024,”amesema Dkt. Chang’a.

Amesema katika msimu huo wa mvua za vuli,msimu unatarajiwa kutawaliwa na vipindi virefu vya ukavu na mtawanyiko wa mvua usioridhisha ambapo ongezeko kidogo la mvua linatarajiwa kujitokeza katika baadhi ya maeneo hususan mwezi Disemba 2024.

” Katika Mifumo ya hali ya hewa katika msimu huo,Joto la bahari la chini ya wastani linatarajiwa ktaika eneo la kati la kitropiki la bahari ya Pasifiki,hali inayoashiria uwepo wa La-Nina,hivyo Joto la bahari la Juu Kidogo ya wastani linatarajiwa katika eneo la mashariki mwa Bahari ya Hindi,”amesema.

Dkt.Chang’a amesema hali hiyo inatarajiwa kupunguza kasi ya msukumo wa unyevu nyevu kutoka bahari ya hindi kuelekea nchini hasa katika maeneo ya ukanda wa pwani na nyanda za juu Kaskazini Mashariki.