January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TMA chachu kusaidia kupunguza athari za kuzama maji nchini

Na Mwandishiwetu, Timesmajira.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetajwa kuwa chachu ya kupunguza athari za kuzama maji nchini kwenye mkutano na waandishi wa habari uliyoandaliwa na Shirika la Usimamizi wa Mazingira na Maendeleo (EMEDO) katika ukumbi wa hoteli ya Mbezi Garden, tarehe 24 Julai 2024.

Mkutano huo ni moja ya maandalizi ya kuadhimisha Siku ya Kuzama Maji Duniani (World Drowning Day) ambayo huadhimishwa kila mwaka tarehe 25 Julai.

Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi Mtendaji wa EMEDO, Editrudith Lukanga amezipongeza taasis za Serikali kwa kushirikiana na EMEDO, huku akiitaja TMA kama Taasisi ambayo imekuwa chachu katika kusaidia kupunguza athari zitokanazo na hali mbaya ya hewa na hivyo kuepusha jamii kuzama maji.

“Kupitia ushirikiano kati yetu na taasis mbalimbali za serikali, TMA imekuwa chachu katika kusaidia kupunguza athari zitokanazo na hali mbaya ya hewa na kuepusha jamii kuzama maji”.

Alisema Editrudith Lukanga.Kwa upande mwingine Afisa Mkaguzi wa Vyombo Majini (TASAC), George Mnali ameelezea utaratibu wao katika kukabiliana na hali mbaya ya hewa mara baada ya kupata taarifa za TMA, kazi yao ni kuzichakata kulingana na matumizi yao katika kuhakikisha wanapunguza athari zinazoweza kujitokeza Baharini au Ziwani.

Aidha, Mtaalam wa hali ya hewa mwandamizi kutoka TMA, Aloyce Swenya, alielezea huduma mbalimbali zinazotolewa na Mamlaka na kuishukuru taasis ya EMEDO kwa kuendeleza ushirikiano huku akiwasisitiza wadau wengine kuhamasika katika utumiaji wa taarifa za hali ya hewa ikiwemo huduma mahususi zinazotolewa na TMA ili kuleta maendeleo endelevu hapa nchini.