December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TIRDO waja na Teknolojia ya kuzalisha mafuta ya parachichi

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) ni moja kati ya mashirika ya kitafiti yanayoshiriki Maonesho ya Kilimo na Mifugo maarufu kama Nane yanayofanyika Kitaifa katika Viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.

Katika Monesho hayo TIRDO kama shirika la Utafiti nchini wamekuja na tafit mbali mbali mojawapo ni mashine ya kukamua mafuta yanayotokana na matunda ya Parachichi(Avacado) mafuta ambayo mbali na kuwa na soko kubwa ndani na nje ya nchi lakini pia ni njia mojawapo ya namna bora ya kuongeza thamani ya mazao hapa nchini.

Mtafiti na Mtaalam wa Mitambo Paul Josephat Kimath amesema mashine hiyo imebuniwa na kutengenezwa na wataalam wa TIRDO asilimia mia moja na kuwa wamefanya utafiti na kujiridhisha kuwa mashine hiyo ina ubora na itawasaidia wakulima wanaozalisha Parachichi kupata soko la bidhaa zao na kuwapa faida kubwa.

Bwana Kimathi ameongeza kuwa Mashine hiyo ina uwezo wa kuchakata parachichi kavu hadi kilo 120 kwa siku na hivyo kumpatia mzalishaji kati ya Lita 30 hadi 40 kwa siku.Bwana Kimathi amesema kwa sasa mafuta ya Parachichi yanauzwa kati ya shilingi 20,000 hadi 35,000 kwa lita jambo ambalo litaongeza thamani ya mazao kwa kiasi kikubwa.

Mmoja wa watembeleaji katika banda la TIRDO Bwana Joseph Lilo kutoka Wilaya ya Rungwe alifurahishwa na teknolojia hii na amewakaribisha wataalam wa TIRDO katika Wilaya yao kwa ajili ya kuwapa elimu kutokana na matunda hayo kukosa soko katika Wilaya yao ya Rungwe.

Maonesho ya nane nane yalianza rasmi tarehe Moja Agosti na yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 8 Agosti 2023.