December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tigo wazindua kili half marathon 2023

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Meneja Mawasiliano wa Kampuni ya Tigo, Woinde Shisael amesema Tigo inajivunia kuwa mmoja wa wadhamini wa Mbio za kimataifa za Kilimanjaro Premium Lager Marathon kwa mwaka 2023 kwani mbio hizo huitangaza Tanzania kwa kuwakutanisha washiriki zaidi ya 12,000 kutoka nchi takribani 55, na kupelekea kukuza vipaji na uchumi wa Taifa.

Woinde ameyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa mbio hizo ambazo zinatarajiwa kufanyika Februari 26, 2023 ikiwa ni toleo la 21 tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo.

“Kama kampuni ya mawasiliano, tumekuwa wadhamini wa Tigo Kili Half Marathon kwa mwaka wa 8 kutokana na ukweli mashindano haya yamekuwa ni jukwaa muhimu katika kukuza vipaji, uchumi wa taifa pamoja na uhifadhi wa mazingira hususan maeneo ya Mlima Kilimanjaro”

Woinde amesema mashindano hayo yanaendelea kukua kila mwaka huku yakiteka hisia za washiriki wengi wakiwemo wanariadha mahiri wa kimataifa kutoka sehemu mbalimbali duniani.

“Washiriki wanaotaka kubadilishana matukio, mandhari na uzoefu wa Tigo Kili Half Marathon – 2023 wanapaswa kujiandikisha kupitia Tigo Pesa na kupata nafasi ya kujishindia zawadi nzuri katika kampeni inayoendelea ya Wakishua Twenzetu Qatar na Hisense,” alisema.

kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Klilimanjaro, Nurdin babu, ambaye aliwakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Same, Edward Mpogolo, amesema mbio za Kilimanjaro Marathon zimeendelea kutoa mchango mubwa katika kukuza sekta ya utalii kwa kupitia utalii wa michezo na hivyo kuungana na Serikali katika kukuza sekta ya utalii nchini.

“Nawapongeza wadhamini wote wakiongozwa na mdhamini mkuu Kilimanjaro Premium Lager, Tigo -21km Half Marathon na Grand Malt -5 km Fun Run kwa mchango wenu mkubwa, bila nyinyi na wafadhili wengine wote pamoja na washiriki, mafanikio haya yasingeonekana”

Mkuu huyo wa mkoa ametoa wito kwa washiriki Watanzania kujiandaa na mashindano hayo ya kimataifa ili kuhakikisha zawadi nyingi zinabaki nyumbani lakini pia amewataka washiriki na mashabiki kutumia msimu wa Marathon kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii miongoni mwao vikiwemo Mlima Kilimanjaro, Serengeti, Ngorongoro, Zanzibar na vivutio vingine.

Kwa upande wake, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Irene Mutiganzi, ambaye pia ni Meneja wa Chapa ya Grand Malt, alisema wao kama wadhamini wakuu wanajivunia kuwa sehemu ya mafanikio katika sekta ya michezo hapa nchini kupitia Kilimanjaro Marathon, ambayo amesema ni tukio kubwa ambalo kwa kutimiza miaka 21 limechukua muda mrefu tangu kuanzishwa kwake.

Nao Waandaaji wa hafla hiyo walitoa wito kwa washiriki kuchukua fursa ya punguzo la ada ya kiingilio lijulikanalo kama Early Bird kuanzia tarehe 24 Oktoba hadi usiku wa manane tarehe 15 Desemba ambapo, baada ya hapo viingilio vitaendelea kuwa vile vya kawaida ambavyo alisema havitakuwa na punguzo na kwamba tiketi zitaendelea kuuzwa kati ya Desemba 16, 2022 hadi saa sita usiku tarehe Februari 6, 2023 au pale idadi ya washiriki wa kipengele hicho itakapotimia.