Na Penina Malundo, Timesmajira
RAIS wa Zamani wa Afrika Kusini,Thabo Mbeki amesema changamoto inayolikumba bara la Afrika si ukosefu wa sera nzuri bali ni uhaba wa viongozi wenye uwezo wa kuzitekeleza.
Pia amesisitiza umuhimu wa viongozi wa bara la Afrika kuweka mikakati thabiti itakayoweza kusaidia kuzalisha ujuzi utakaosaidia kukuza uchumi katika bara hilo.
Ameyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa Mhadhara wa 15 wa siku ya Afrika ya Thabo Mbeki amesema bara la Afrika lina maono makubwa, lakini hatua za kuyafanikisha hazipo kwa kiwango kinachohitajika.
Amesema licha ya bara la afrika kuwa na viongozi wazuri bado wanachangamoto ya uthubutu wa utekelezaji wa sera na mikakati inayoweza kuleta matunda.
”Maendeleo ya Bara ya Afrika yatapatikana iwapo viongozi wataweka mbele maslahi ya nchi zao na kuongoza kwa uwazi,uadilifu na dhamira ya dhati ya kuleta mabadiliko chanya kwa waafrika wote.
”Afrika ina utajiri na uwezo mkubwa lakini mafanikio haya yanahitaji viongozi wenye maono,wawajibikaji na wanaotanguliza maslahi ya wananchi wao badala ya matakwa binafsi,”amesema

Akizungumzia kuhusu Taasisi yake alisema kutokana na ushauri kutoka kwa marafiki zake,alianzisha Taasisi ya Uongozi wa Afrika kupitia Chuo Kikuu cha Afrika Kusini (UNISA).
Amesema ni Taasisi yenye lengo la kuwajengea uwezo viongozi wa Afrika ili waweze kusimamia na kutekeleza sera mbalimbali zinazolenga maendeleo barani humo.
Mbeki amesema taasisi hiyo inafika zaidi ya nchi 40 za Afrika huku shughuli zake ni kuendesha mihadhara ya Siku ya Afrika ambapo uzunguka katika nchi mbalimbali kwa lengo la kuzungumzia masuala ya maendeleo ya bara la Afrika.

Akizungumza katika Mkutano huo,Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Balozi Mahmoud Thabit Kombo anasisitiza kila mwafrika anapaswa kutafakari mafanikio changamoto na matarajio ya maendeleo ya bara la Afrika kwa msingi wa amani na utulivu.
Anasema kuna umuhimu wa kuwaenzi viongozi waliotangulia kwa kudumisha fikra za Uafrika,pamoja na kuendeleza mapambano ya ukombozi wa kiuchumi na mshikamano wa Afrika,kama urithi wa kizazi cha sasa na kijacho.

Naye Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, anasema kuwa bara la Afrika lina kila sababu ya kuimarisha mshikamano na umoja kwa kuunganisha juhudi za taasisi mbalimbali zinazolenga kudumisha amani, maendeleo, na urithi wa fikra za viongozi wakuu wa Afrika.
“Kuanzia leo, taasisi hizi mbili lazima zishirikiane kwa karibu na hili ni azimio rasmi la Bodi,Tunataka kuhakikisha kazi na fikra za Mwalimu Julius Nyerere na Rais Thabo Mbeki zinaenziwa, kuendelezwa, na kuhifadhiwa kwa ajili ya vizazi vijavyo,” amesema Butiku.

Anasema kuwa taasisi hizo zimekubaliana kushirikiana kukusanya nyaraka, machapisho, hotuba, na kazi za sanaa zinazohusiana na maisha na fikra za viongozi wakuu wa Afrika, zikiwemo picha, vibonzo, na filamu fupi za kihistoria.
Butiku ametumia fursa hiyo kuonya juu ya athari za mipaka ya kikoloni barani Afrika, akisema migogoro mingi ya kikabila inachochewa na mipaka ya kiholela iliyowekwa na wakoloni bila kuzingatia muundo halisi wa kijamii na kitamaduni wa watu wa Afrika.
Aidha Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo,Palamagamba Kabudi anasema ili bara la Afrika liweze kupaa zaidi katika nyanja mbalimbali linapaswa kuzingazia mambo muhimu ikiwemo kuwa na juhudi za pamoja katika kujenga mataifa imara yenye maendeleo endelevu na kutoa huduma bora kwa raia wake.
Anasema juhudi hizo zinatakiwa kujikita katika kuboresha na kuimarisha taasisi,uchumi,miundombinu ,utawala,sheria ,elimu,afya na sekta nyingine muhimu katika kila taifa ili kuhakikisha ustawi wa wananchi na ufanisi.
More Stories
Dkt.Biteko:Wazazi msiwahusishe watoto kwenye migogoro yenu
Waziri Lukuvi amuwakilisha Rais Samia Tabora
Thabo Mbeki aipongeza Tanzania kuandaa mhadhara wa UNISA mara tatu mfululizo