Na Penina Malundo,Timesmajira
KAMPUNI ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC),imetoa wito kwa wananchi waishio katika vijiji vya Nsongwi Juu, Nsenga na Mbeye1 juu ya umuhimu wa utunzaji wa Mradi wa Jotoardhi Ngozi na Miundombinu yote iliyowekwa.
Akitoa rai hiyo hivi karibuni Afisa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano TGDC,Khadija Ahmed wakati wa ziara ya wataalam kutoka TGDC iliyoanza Machi 17 hadi 20, 2025 katika vijiji hivyo yenye lengo la uhamasishaji na uelimishaji katika vijiji hivyo ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kuimarisha uhusiano na jamii zinazouzunguka mradi wa Jotoardhi Ngozi.
Ahmed amesema kila mmoja anapaswa kuwa mlinzi wa mazingira katika eneo hilo na kuhakikisha wanatunza miundombinu ya mradi ikiwa ni safari kuelekeza uzalishaji umeme utokanao na rasilimali ya jotoardhi.

” Tumekuja katika vijiji hivi kwa ziara ya mfululizo kwa nyakati tofauti ambapo wakazi wa maeneo haya walinufaika,tumetoa elimu kwa wananchi wa vijiji hivi vitatu na wao wameonyesha utayari wao katika kuipokea na kuilinda miundombinu inayozunguka miradi ya jotoardhi.
”Moja ya eneo tuliloongelea ni pamoja na elimu ya ufahamu na umuhimu wa utunzaji wa mradi pindi shughuli za uchimbaji zitakapoanza kwa ajili ya uhakiki wa rasilimali ya jotoardhi ikiwa ni safari kuelekeza uzalishaji umeme utokanao na rasilimali ya jotoardhi,”amesema.

Amesema miongoni mwa Kampeni ya TGDC inayoendesha ni pamoja na utunzaji wa mazingira hivyo hata mradi huo wa umeme wa jotoardhi utakapozalishwa hautachafua mazingira bali utakuwa ni mradi rafiki wa mazingira.

”TGDC iko mbioni kuhakiki rasilimali ya jotoardhi katika miradi ya kipaumbele mitano ya Ngozi na Kiejo-Mbaka (Mbeya), Songwe (Songwe), Luhoi (Pwani) na Natron (Arusha) yenye lengo la kuzalisha Megawati 200 za umeme ifikapo 2030.
”Kwa sasa itaanza na mradi wa jotoradhi Ngozi (70Mw) ambapo baada ya uhakiki,hatua ya uzalishaji itafuata na kwa kufanya hivi, TGDC itakuwa imechangia umeme kwenye gridi ya Taifa unaotokana na nishati safi isiyoharibu mazingira.”amesema.

Kwa upande wa Mmoja wa wananchi wa Kijiji cha Nsongwi Juu,Ally Girson ameishukuru TGDC kwa elimu waliyoitoa kwa wakazi wa eneo hilo huku wakisisitiza suala la unufaikaji kwao katika upande wa ajira na uboreshwaji wa miundombinu ya barabara, mambo ambayo yalitolewa ufafanuzi kwa kuhakikishiwa ajira pamoja na uboreshaji wa barabara.
Ameomba kuhakikishiwa ajira za muda wakati wa utafiti na za moja kwa moja wakati wa uzalishaji, uboreshwaji miundombinu pamoja na mashirikiano baina ya TGDC na wananchi.

Naye Mwananchi kutoka kijiji cha Mbeye 1,Sister Aloni ameishukuru TGDC kwa namna ambavyo imekuwa mstari wa mbele kuunga mkono shughuli za jamii ya wana Mbeye1 ikiwemo kupeleka maji katika Shule ya Msingi Mbeye1, jambo lililowapunguzia ajali wanafunzi waliokuwa wakivuka barabara kwa ajili ya kufata maji.
Pia ameshukuru ugawaji wa mabegi kwa wanafunzi wa shule hiyo pamoja na vifaa kama daftari huku akisisitiza kuwa mabalozi wazuri wa ulinzi wa miundombinu hiyo na kulaani uharibifu wa miundombinu ambao hufanywa na watu wasio waaminifu.

Wataalamu wengine kutoka TGDC waliotoa elimu katika kijiji hicho ni pamoja na Mhandisi Esther Range, Juma Mpamba, Boaz Mazigo, Joshua Nelei,Omary Seleman na Leonce Komba
More Stories
Prof.Muhongo apongezwa kuleta majadiliano sekta ya elimu Musoma
Ntiboneka:Mashirika wekezeni katika kubadilisha fikra za vijana,wanawake
Simbachawene:Watendaji wakuu acheni kuwaona wakaguzi wa ndani kama maadui