Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Magharibi imejipanga vizuri ili kuhakikisha rasilimali za misitu na vyanzo vya maji vilivyopo katika Kanda hiyo vinalindwa ipasavyo.
Hayo yamebainishwa juzi na Kamanda wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) Kanda ya Magharibi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi (TFS) Kanda ya Magharibi Ebrantino Migiye alipokuwa akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake.
Amesema kuwa serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan inastahili pongezi kwa juhudi kubwa inazoendelea kufanya ili kuhakikisha rasilimali zote zilizopo katika maeneo ya misitu ya hifadhi haziharibiwi.
Ameongeza kuwa uamuzi wa Rais Samia wa kuridhia baadhi ya vijiji vilivyokuwa katika maeneo ya hifadhi kurasimishwa na kutambulika rasmi kisheria ni wa kupongezwa sana.
Kamanda Mgiye amesema awali vitendo vya uvamizi holela vilichochea kwa kiasi kikubwa uharibifu wa vyanzo vya maji na rasilimali zilizopo kutokana na wingi wa shughuli za kibinadamu zilizokuwa zikifanyika, lakini sasa hali ni shwari.
Amefafanua kuwa hatua hiyo imepunguza kwa kiasi kikubwa vitendo hivyo na kuongeza kuwa wataendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya matumizi sahihi ya rasilimali hizo na kuzuia mianya yoyote ya uharibifu.
‘Misitu ni uhai, ikitunzwa vizuri itakuwa msaada mkubwa kwa wananchi, maisha ya binadamu yanategemea sana miti kwa matumizi mbalimbali ikiwemo kupata mvua za kutosha’, amesema.
Kamanda Mgiye amsema katika kuhakikisha rasilimali hizo zinakuwa salama wameendelea kufanya kampeni ya upandaji miti tangu mwaka 2020 na kudhibiti ukataji miti ovyo ili kulinda mazingira na kurejesha uoto asali.
Aidha ameongeza kuwa wataendelea kukabiliana na majanga asilia ya ardhi na kusaidia jamii ili kuhakikisha rasilimali misitu inaendelea kupata hewa ya ukaa ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
‘Tumeedelea kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu kupanda miti ya kutosha katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Tabora ili jamii ipate mvua za kutosha na kuimarisha ulinzi wa vyanzo vya maji’, alibainisha.
Mgiye ameeleza kuwa kampeni hiyo inatarajiwa kufanyika mapema mwezi Januari mwaka huu ili kuunga mkono Kampeni ya Siku ya Mazingira ya Misitu Duniani ambayo inaadhimishwa Machi 1 huku akibainisha lengo kuu la kampeni hiyo kuwa ni kurejesha uoto wa asili katika misitu yote ya hifadhi.
Amewashukuru wanahabari kwa kuendelea kuelimisha jamii umuhimu wa upandaji miti katika maeneo yao na kuwataka wananchi na taasisi mbalimbali kujitokeza kwa wingi kuchukua miti hiyo na kuipanda.
More Stories
CP.Wakulyamba ashuka Katavi na Nguzo nne za Uongozi
Zanzibar kuzalisha wachezaji wenye vipaji
Maandalizi ya mkutano mkuu CCM yapamba moto