December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TET yaingia makubaliano na Shirika la Educate

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

TAASISI ya Elimu Tanzania (TET) wameingia makubaliano ya ushirikiano na
Shirika la Educate kwa ajili ya kuimarisha utoaji wa Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini (MEWAKA) ambapo mafunzo
hayo yataimarishwa katika somo la biashara.

Lengo la makubaliano hayo ni kuwawezesha walimu kufundisha somo hilo kwa kutumia mbinu za kisasa na
kuwa na maarifa yanayoendana na wakati katika ufundishaji wa somo hilo.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi TET, Aneth
Komba wakati akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam.

Alisema kupitia lengo hilo, walimu wa somo la biashara watapata mafunzo kupitia mfumo unaojulikana kama
Learning Management System.

“MEWAKA tunatoa mafunzo haya kuhakikisha walimu wote wanakuwa wanatumia mbinu zina zoendana na wakati kwa kufundisha masomo
yao na yanatolewa kwa kutumia mfumo wa Learning Management System ambao
umeandaliwa na TET,”alisema.

“Mfumo huu unapatikana bure, tumesaini makubaliano na Airtel, hivyo walimu wanaweza kupata nyaraka zote za kuweza kujifunzia kwa mfumo huu bila kuwa na
gharama yoyote.”

Pia alisema makubaliano hayo yana lengo la kusaidia utekelezaji wa mafunzo ya
walimu kazini kwa ngazi ya elimu ya Sekondari ambapo pia wanaanzisha programu ya kuajiri walimu wa kujitolea kwa somo la biashara.

“ Tunaisaidia Serikali kupunguza ombwe la walimu wa somo la biashara, hivyo
shule chache zitakazoonekana
zina uhitaji mkubwa makubaliano yetu yatasaidia kuweza kuajiri walimu kwa
mkataba katika somo hilo,”
alisema.

Aidha, alisema makubaliano hayo yana lengo la kuisaidia TET kufanya safari za
kimafunzo nje na ndani ya nchi kwa lengo la kujifunza ili kuhakikisha wanafunzi
wanashindana kitaifa na kimataifa.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Educate, Kamanda Kamiri, alisema safari ya ushirikiano baina yao ilianza mwaka 2022 nchini Rwanda ambapo
ilikuwa safari ya mafunzo.

Alieleza kuwa kwa kuanza wameanza na masomo ya biashara lengo likiwa na
kuwatengenezea wanafunzi mazingira ya kuongeza ujuzi zaidi katika sekta ya biashara ili kukuza soko la ajira kupitia
kujiajiri wenyewe.