Na Iddy Lugendo, Timesmajira Online
TEMESA yaingia ushirikiano baina yao na Azam Marine ambao utawawezesha kutumia vivuko vya Azam Marine kwaajili ya kupunguza kero kwa wananchi wa Kigamboni Jijini Dar es Salaam wakati wakiendelea kufanya ukarabati wa vivuko vyao.
Akizungumza baada ya kufanya makubaliano hayo leo Juni 13,2022 Jijini Dar es Salaam Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Lazaro N. Kilahala amesema wamekabidhiwa vivuko viwili ambavyo kila kimoja kinauwezo wa kubeba watu 250 kwa wakati mmoja hivyo basi kupitia vivuko hivyo vitaweza kufanya safari nyingi kwa siku kuliko vivuko vya kawaida kwani ni vivuko ambavyo vinatembea kwa haraka zaidi.
Amesema kuna gharama ambazo wamekubaliana na Azam wao kama TEMESA watalipa lakini kwa watumiaji wa huduma hiyo wataendelea kulipa gharama zilezile na wao kama TEMESA watajua ni namna gani wanaweza kumalizana na Azam.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Azam Marine Aboubakar Salim amesema wameona kuna umuhimu mkubwa wa kuingia makubaliano na TEMESA kwasababu kumekuwa na changamoto ya vivuko kwa upande wa Magogoni na Kigamboni kupitia makubaliano hayo watawez kupunguza kero hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Fatma Nyangasa ameipongeza Azam Marine kwa kukubali ushirikiano huo kwani watasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza kero ya vivuko kwenye eneo la Kigamboni.
Aidha amesema Serikali imekuwa ikiendelea kufanyia kazi changamoto moja baada ya nyingine ndo maana wakaamua kuingia makubaliano na Kampuni ya Azam Marine ikiwa ni moja wapo ya kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
“Serikali tayari imekwisha tenga fedha kwaajili ya kununua kivuko kikubwa zaidi ya Mv Magogoni ambayo itakuwa inauwezo wa kubeba abiria wengi zaidi pamoja na vyombo vingi vya usafiri kwa wakati mmoja”. Amesema Nyangasa.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja