September 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TEF yawatoa wasiwasi wadau wa Habari

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Mwenyekiti wa Jukwaaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amewataka waandishi na wadau wa habari nchini, kuendelea kuwa na subira katika kusubiria uwasilishwaji wa muswada wa Sheria ya Habari utakaosomwa kwa mara ya kwanza bungeni mwaka huu.

Amesema kuwa mwezi huu jukwaa hilo linatarajia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari itawasilisha Bungeni Muswada wa Huduma za Habari ili ujadiliwe na hatimaye kupitishwa na kuwa Sheria.

Akizungumza na gazeti la Majira, February 03,2023 jijini Dar es Salaam Balile ameweka wazi kuwa jukwaa la wahariri lina matumaini makubwa kuwa kujadiliwa kwa muswada huo kutasaidia kuboresha sheria mbalimbali za habari ili kutoa fursa kwa waandishi na wadau wa habari kuwa na uhuru wa kujieleza

“Nimeona watu wengi wanaangalia ratiba ya bunge wananitumia maswali, wananipigia simu kwamba vipi mbona haumo kwenye sheria zitakazojadiliwa, mimi ninazo taarifa za uhakika kwamba mpaka jana jioni kulikuwa na kila dalili kwamba muswada utaingizwa bungeni” Amesema balile

Aidha ameongeza kuwa anadhani muswada huo utaingia katika utaratibu wa marekebisho madogo ya sheria mbalimbali zijulikanazo kama “miscellaneous amendments” hivyo jukwaa hilo linaendelea kuwasiliana na mamlaka za serikali na watunga sera ili kuhakikisha utekelezaji wa majadiliano ya muswada huo.

“Nadhani hatutaona ule muswada kwa njia ya kawaida ambapo unapelekwa muswada unaojitegemea, kutakachotokea muswada huu utaingia katika utaratibu wa marekebisho madogomadogo ya sheria mbalimbali”