November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TCU yaongeza muda udahili wa shahada ya kwanza katika Taasisi za Elimu ya juu

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Tume ya vyuo vikuu Tanzania (TCU) imesema udahili katika awamu zote tatu kwa ngazi ya shahada ya kwanza katika Taasisi ya elimu ya juu nchini kwa mwaka wa masomo 2023/24 umekamilika ambapo majina ya waliodahiliwa katika awamu ya tatu yanatangazwa na vyuo husika.

Aidha TCU imewaasa wananchi kuepuka kutapeliwa na watu wanaojiita mawakala au washauri wanaodai wanatoa huduma ya jinsi ya kujiunga na vyuo vya elimu ya juu nchini.

Hayo yamebainishwa na Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo vikuu Tanzania, Profesa Charles Kihampa wakati akizungumza na waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam akitoa taarifa kuhusu kuongeza muda wa udahili wa shahada ya kwanza katika Taasisi za Elimu ya juu nchini kwa progwamu ambazo bado Zina nafasi kwa mwaka wa masomo 2023/24.

Aidha TCU imewaelekeza Waombaji udahili wa shahada ya kwanza kuwa masuala yote yanayohusu udahili au kujithibitisha katika chuo kimoja yawasilishwe Moja kwa moja kwenye vyuo husika.

Kwa upande wa Waombaji waliodahiliwa katika chuo zaidi ya kimoja katika awamu ya tatu na wale ambao hawakuweza kuthibitisha udahili katika awamu zilizopitwa, wamehimizwa kuthibitisha udahili wao katika chuo kimoja wapo kuanzia tarehe 13 – 24 Octoba.

“Hii watatumia namba maalumu ya Siri iliyotumwa kwa ujumbe mfumbe kupitia namba zao za simu au barua pepe walizotumia wakati wa kuomba udahili”

“Wale ambao hawatapata kwa wakati ujumbe huo nawashauri kuingia kwenye mifumo ya udahili ya vyuo walivyodahiliwa na kuomba kutumiwa ujumbe mfupi wenye namba maalumu ya Siri ili kuweza kujithibitisha katika chuo husika”

Kuhusu kufunguliwa kwa awamu ya nne ya udahili Prof. Kihampa amesema Tume imeongeza muda wa udahili kwa kufungua awamu ya nne na ya mwisho ya udahili iliyoanza Jana Oktoba 13-17, 2023 na kusisitiza kuwa Waombaji ambao hawakuweza kutuma maombi ya udahili au hawakufanikiwa kudahiliwa katika awamu zilizopita kutokana na sababu mbalimbali watumie fursa hiyo kwa kutuma kwa usahihi maombi yao ya udahili kwenye vyuo wanavyovipenda.

“Tume imepokea maombi ya kuongeza muda wa kutuma maombi ya udahili kutoka kwa Jumuhiya ya wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya juu Tanzania (TAHLISO) baadhi ya Waombaji ambao hawakufanikiwa kupata udahili katika awamu zilizopita na pia vyuo ambavyo bado vina nafasi hivyo Waombaji watumie vizuri fursa hii”

Prof. Kihampa ameutaja utaratibu wa udahili katika awamu ya nne kwa mwaka wa masomo 2023/24 ambapo alisema “Octoba 13-17, 2023 kutakuwa na tukio la kutuma maombi ya udahili katika awamu ya nne, Octoba 21-22, 2023 vyuo kuwasilisha Tume majina ya waliodahiliwa katika awamu ya nne, Octoba 25, 2023 Vyuo kutangaza majina ya waliodahiliwa katika awamu ya nne lakini pia Octoba 25 Hadi 27 , 2023 kuthibitisha udahili kwa waliodahiliwa zaidi ya chuo kimoja katika awamu ya nne na wale walioshindwa kuthibitisha udahili wao katika awamu za udahili zilizopita.”

Prof. Kihampa amezielekeza Taasisi zote za Elimu ya juu nchini zinazofanywa udahili wa shahada ya kwanza kuendelea kutangaza programu ambazo bado Zina nafasi.