January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TCRA yatoa adhabu kwa kampuni sita za simu

Na Irene Clemence,TimesMajira Online, Dar

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa adhabu kwa kampuni sita za simu za mkononi na kuzitaka kulipa faini ya shilingi Billioni 38,129,320,840.50 kutokana na kutoa huduma chini ya kiwango kwa watumiaji wa simu za mkononi.

Pia imeziagiza kampuni hizo kutumia fedha hizo za faini walizotozwa katika adhabu kuwekeza katika kuboresha zaidi huduma zao ndani ya siku 90 badala ya kuzipeleka katika mamlaka hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurungezi Mkuu wa TCRA, Mhandisi James Kilaba amesema, katika kipindi cha mwezi Oktoba, Novemba na Desemba mwaka jana TCRA ilipima ubora wa huduma za mawasiliano ya simu ya mkononi kufanya upimaji katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Singida, Kilimanjaro, Mbeya, Unguja, Tanga, pamoja na Simiyu na kubaini kasoro hizo.

Akizitaja kampuni zilizopewa adhabu ni pamoja na Airtel Tanzania plc(AIRTEL) ambapo imetakiwa kulipa sh. Billioni 11,519,775,721.58, Mic Tanzania Plc (TIGO) Billioni 13,032,049,305.32, Viettel Tanzania Plc (Halotel)Billioni 3,409,107,801.61, Vodacom Tanzania plc( Vodacom) Bilioni 7,810,714,298.68, Zanzibar Telecom Plc (Zantel) Billioni 1,021,407,142.89 pamoja TTCL Corporation (TTCL) Billioni 1,336,266,570.42.

Amesema, kabla ya kuchukua hatua hizo TCRA iliwataka watoa huduma kufika ofisini Januari 11 hadi 13 ili kujieleza kwa nini wasichukuliwe hatua za kisheria kwa kushidwa kufikia vigezo vyote vya ubora wa huduma.

Mhandisi Kilaba amesema, kupitia vigezo 11 ya matokeo ya upimaji huo ulibainisha kwamba watoa huduma wote hawakufikia baadhi ya vigezo vya viwango vya huduma vya ubora wa huduma kama vilivyoanishwa katika kanuni za ubora za huduma za mwaka 2018 kwa viwango mbalimbali.

“Kwa mujibu wa kanuni ya 29 ya kanuni, mtoa huduma anayeshidwa kufikia vigezo vya ubora vya huduma anawajibika kulipa faini za viwango mbalimbali,”amesisitiza Mhandisi Kilaba.

Amesema kwa kuzingatia utetezi uliotolewa na watoa huduma TCRA imejiridhisha kuwa watoa huduma hao wamekiuka kanuni za ubora wa huduma na kwa mujibu wa kifungu cha 48(2)&(3) cha Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania sura ya 172 marejeo ya mwaka 2017 ya sheria za Tanzania.

Amesema, vigezo ni pamoja na upimaji huo uliangalia katika eneo la upatikanaji wa mtandao, kiwango cha simu zilizoshindikana kuunganishwa, kiwango cha simu zilizokatika, muda wa kuunganishwa simu iliyopigwa, wigo wa upatikanaji wa huduma pamoja na kiwango cha simu zilizofanikiwa kuunganishwa.

Ameongeza kuwa, maeneo mengine ni pamoja na kuangalia kiwango cha uwezo wa minara kupotezana mawasiliano, wastani wa muda unaotumika katika kupakia na kupakua data, uwiano wa muunganisho wa data pamoja na upatikanaji wa huduma za jumbe mfupi.

Katika hatua nyingine TCRA imemtaka kila mtoa huduma kuwasilisha mpango wa kimaandishi ndani ya siku tatu wa namna atakavyotumia fedha hizo za faini katika kuboresha huduma zake kama alivyoelekezwa.

Aidha, amewaomba watoa huduma kuendelea kuchukua hatua za makusudi za kuboresha huduma ili kukidhi viwango vya ubora kwa mujibu wa kanuni ya 9,10 na 11 za mawasiliano ya kielektroniki na Posta.

Vilevile amesema endapo mtoa huduma yoyote atashidwa au kukataa maagizo hayo TCRA itachukua hatua zaidi za kudhibiti na kisheria pasipo kutoa taarifa zaidi kwa mtoa huduma husika.