November 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TCRA wapewa miezi mitatu kumaliza changamoto za bando, vifurushi

Na Prisca Ulomi, WMTH

WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile ametoa miezi mitatu kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kumaliza changamoto za bando na vifurushi
zinazotolewa na kampuni za simu za mkononi kwa wananchi.

Dkt. Ndugulile ameyasema hayo alipotembelea TCRA ikiwa ni moja ya taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo kwa lengo la kufahamiana, kutambua majukumu yao na kuzungumza na Bodi, Menejimenti na wafanyakazi wa taasisi hiyo ili kuwa na uelewa wapamoja na kushirikiana kwa kufanya kazi kwa pamoja katika kuhudumia wananchi kuelekea Mapinduzi ya Nne ya Viwanda na kuiwezesha Tanzania kuwa na uchumi wa kidijitali.

Amesema, ni lazima TCRA ishughulikie malalamiko ya wananchi kwa kuwa wananchi hawana
imani na vifurushi na bando, na kuwe na mfumo wa kuhakiki gharama halisi za mawasiliano
kuendana na fedha aliyotoa mwananchi na kuwe na namba ya bure ambayo wananchi
watapiga ili kuwasilisha malalamiko yao ili kuwawezesha wananchi kuongeza imani yao kwa
Serikali.

“Ni heri tufanye maamuzi mabaya kuliko kutokufanya maamuzi, nataka mshirikiane na Baraza la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA – CCC) kumaliza changamoto hii kwa kuwa Watanzania sio wajinga, nataka aone kapata shilingi moja anaitumia shilingi moja yake kupiga simu,” amesema Dkt. Ndugulile.

Pia, amewataka kuhakikisha kuwa, chaneli tano za bure za runinga zinaonekana hata baada
ya muda wa kulipia kumalizika kwa kuwa chaneli hizo hazionekani kwenye baadhi ya
ving’amuzi.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhandisi Kundo Mathew ameipongeza TCRA kwa
kutengeneza mifumo ya TEHAMA, kutambua changamoto zilizopo na imejipanga kuzifanyia
kazi kwa kuwa lazima TEHAMA ichukue nafasi yake na itufikishe watanzania tunakotaka
kwenda

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula amewataka wafanyakazi wa TCRA
kujiongeza na kujituma zaidi badala ya kusubiri maagizo na maelekezo kwa kuwa wao ni
wataalamu, hivyo washirikiane kwa pamoja ili kuhakikisha kuwa wanaendelea
kuwahudumia watoa huduma na watumiaji wa huduma za mawasiliano.

Hata hivyo Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Mhandisi James Kilaba amekiri kuwepo wa changamoto za
bando na vifurushi na ameahidi kuzifanyia kazi kwa kuwa TEHAMA imeongeza mnyororo wa
thamani kwenye sekta zote na imesogeza huduma mbali mbali viganjani.