Na Mwandishi wetu
Benki ya Tanzania Commercial Bank (TCB)imewazawadia washindi wawili safari ya kwenda Zanzibar na malazi waliofanya miamala mingi katika msimu wa wapendanao kupitia kampeni iliyoendeshwa na benki hiyo ijulikanayo kwa jina la Mahaba Kisiwani.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Adam Mihayo, Mkurugenzi wa Biashara za Wateja Wadogo na Kati, Lilian Mtali amesema TCB imefanikiwa kukuza uelewa na matumizi ya bidhaa zake za kidijitali kwa kuwazawadia wateja hao waliofanya miamala mingi katika msimu wa wapendanao.
Amesema kampeni ya Mahaba Kisiwani inadhihirisha malengo ya kimkakati ya TCB kutumia teknolojia kukuza matumizi ya njia za kidijitali katika kufanya malipo.
![](https://timesmajira.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/IMG-20250214-WA0100-1024x682.jpg)
” Kwa kuwazawadia wateja, Benki ya TCB inapanua wigo wa kutoa huduma za kibenki kwa wateja wake kupitia njia mbalimbali, pamoja na kuwapa hamasa wateja kutumia njia hizi zilizo salama zaidi, zenye ufanisi, na rafiki kwao.
“Kampeni hii ni ushindi wa juhudi zetu za kiuvumbuzi na ushuhuda wa dhamira yetu ya kutoa huduma bora za kidijitali,Kampeni yetu ya Mahaba Kisiwani ilibuniwa ili kuwahimiza wateja wetu kufanya miamala kidijitali huku wakijiongezea nafasi ya kushinda safari ya kwenda wikiendi kisiwani Zanzibar.,”amesema.
![](https://timesmajira.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/IMG-20250214-WA0110-1024x682.jpg)
Mtali amesema mbali na kuwakabidhi zawadi hizo washindi hao pia TCB inaadhimisha hatua muhimu ya miaka 100 ya huduma na ubora wa benki tangu kuanzishwa kwake.
Amewapongeza wafanyakazi wa benki hiyo kwa juhudi na mchango wao katika mafanikio ya benki hiyo. “Mafanikio ya benki yetu katika kipindi cha miaka 100 iliyopita ni matokeo ya juhudi na bidii za kila mmoja wetu.
“Tunadhamiria kuendelea kuboresha mazingira ya kazi ambayo kila mmoja anathaminiwa, anaungwa mkono na kuwezeshwa tunapoendelea kutoa huduma bora kwa wateja wetu,”amesema
Amesema TCB inaendelea kuahidi kuwekeza katika uvumbuzi wa kidijitali na kuongeza ubora kwa wafanyakazi wake ili kuhakikisha mustakabali wenye mafanikio kwa wateja pamoja na wafanyakazi wake.
![](https://timesmajira.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/1001671859-1024x682.jpg)
Kwa upande wake Ofisa Mkuu wa Huduma za Kidijitali na Ubunifu wa TCB, Jesse Jackson, amesema kuwa kampeni hiyo ni sehemu ya mkakati wa benki wa kuongeza matumizi ya mifumo ya kidijitali katika sekta ya fedha.
“Kampeni ya Mahaba Kisiwani ni uthibitisho wa dhamira yetu ya kusogeza huduma za benki kwa wateja kwa njia za kisasa, salama na rahisi. Kwa kuwazawadia wateja wetu, tunawapa motisha zaidi kutumia mifumo hii ambayo inarahisisha maisha yao,” amesema Jackson.
Mmoja wa washindi wa kampeni hiyo, mfanyabiashara Maygrace Nyambuka, aliipongeza TCB kwa huduma zake bora, akieleza kuwa miamala ya kidijitali imerahisisha biashara yake na kumpunguzia gharama za kutuma na kupokea fedha.
More Stories
Kapinga ashiriki kikao cha Mawaziri wa kisekta Arusha
RAS Manyara aomba kipaumbele ujenzi bwawa la Dongo
Mwakagenda:Zao la ndizi liuzwe katika masoko ya kimataifa