December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TCB yashiriki kikao kazi uzinduzi Tamasha la maendeleo ya Filamu na Sanaa nchini

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

BENKI ya Biashara Tanzania (TCB) imeshiriki katika kikao kazi cha uzinduzi wa Tamasha la Kimataifa la Maendeleo ya Filamu na Sanaa Tanzania linalotarajiwa kufanyika mwezi wa Disemba mwaka huu ambalo liloratibiwa na taasisi ya FAGDI (Foundation Ambassadors Gender Development Initiatives) ikishirikiana na Bodi ya Filamu Tanzania.

Tamasha hili linawakutanisha wadau wa filamu,sanaa na wadau kutoka sekta mtambuka katika jukwaa moja kujadili mustakabali wa maendeleo ya sekta hiyo kitaifa na kimataifa.

Akizungumza kwa niaba ya Benki ya Biashara Tanzania mwishoni mwa wiki, Meneja Mkuu wa Kitengo cha Masoko wa Benki hiyo,Janeth Zoya,amesema kuna umuhimu wa tamasha hilo kuendelea kufanyika nchini. “Benki ya TCB tunatambua nguvu iliyo nayo sanaa katika kuleta mabadiliko ndani ya jamii. Sanaa ni zaidi ya burudani, ni chanzo cha kukuza uchumi, kuchochea umoja wa kitaifa na kutambulisha utamaduni wetu duniani. Tasnia ya filamu na sanaa ina uwezo mkubwa wa kutuvusha nje ya mipaka, kusimulia hadithi na urithi wetu, na kuonyesha ufahari wa tamaduni za Kitanzania duniani,” amesema.

Zoya amesema tamasha hili litatoa fursa muhimu ya kuwakutanisha pamoja wadau mbalimbali kujadili mikakati itakayokuza uchumi na maendeleo ya sekta hii. Hivyo, ni vizuri kutumia fursa hii kushughulikia changamoto zinazoikabili sekta, zikiwemo zile zinazohusiana na uwezeshwaji, uelimishaji na upatikanaji wa masoko.

“Tunapaswa kutambua fursa zilizopo mbele yetu – uwezekano wa kufanya ushirikiano kimataifa, matumizi ya majukwaa ya kidigitali ili kuifikia hadhara ya kimataifa na kutengeneza muundo endelevu utakaowezesha mafanikio ya muda mrefu.”amesema

Udhamini wa Benki ya TCB katika uzinduzi huu unaimarisha dhamira yake ya kusaidia miradi mbalimbali inayochangia maendeleo ya utamaduni na uchumi nchini. Benki ya TCB inakusudia kuchangia katika kukuza maendeleo ya sanaa bunifu na sekta hiyo kwa ujumla ambayo inalenga kuchangia uanzishwaji wa sekta mahiri ya sanaa na utamaduni