October 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TCB yaendelea kupanua wigo wa soko nje ya mipaka

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

BENKI ya Biashara Tanzania (TCB),imesema inaendelea na mkakati wake wa kuthibitisha dhamira ya kupanua wigo wa uwekezaji nje ya mipaka ya nchi kwa kuhakikisha wanapanua wigo wa soko la nje.

Pia imesema kuna umuhimu wa mashirika kushirikiana katika muundo wa kibiashara ili kuweza kuwa wabunifu na wenye uwezo wa kubadilika kuendana  na mazingira. 

Akizungumza hayo jana jijini Arusha wakati wa Kikao Kazi cha siku tatu,kilichofunguliwa rasmi na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan na kuwakutanisha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma kujadiliana mikakati mbalimbali ya mageuzi ndani ya taasisi za umma na uwekezaji wenye tija.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya TCB,Adam Mihayo amesema tayari benki yao imepata mafanikio ya hivi karibuni ya kuzinduzi huduma za kibenki kwa Watanzania waishio nje ya nchi (Diaspora Banking) nchini Comoro.

Amesema kwa kufanya hivyo kunaonyesha dhamira ya kutoa huduma za kibenki nje ya mipaka na kuyafikia mahitaji ya watanzania wote dunia nzima,katika dhamira hii, tunatarajia kuwa katika miaka miwili  ijayo tutaipeleka TCB katika Soko la Hisa (Dar es Salaam Stock Exchange), hivyo kumpa kila Mtanzania fursa ya kumiliki hisa na kuwa sehemu ya mafanikio ya taasisi hii,”amesema

Amesema kuna umuhimu wa mashirika kuunda ubia wa kimkakati pamoja na ushirikiano na muungano ili kutumia mtandao wao wa ndani na utaalamu.

“Ni muhimu kutumia uwezo wa mashirika yetu kufanya kazi tukiungana pamoja  kwa kushirikishana takwimu, kupanga mikakati pamoja, na kusadiana katika utoaji wa huduma,”amesema na kuongeza

” Kwa kufanya hivyo, tutaboresha rasilimali zetu na pia tutawapa wateja wetu  huduma bora kulingana na mahitaji yao na kujenga imani yao kwetu.”amesema.

Aidha amesema ushirikiano wa kimkakati katika tafiti na kubadilishana takwimu baina ya taasisi zinazotegemeana zinaweza kuwasaidia kufikia malengo yao na kuzifanya taasisi hizo kufanya vizuri sokoni.

Mihayo ametoa wito kwa taasisi na mashirika ya umma kutobweteka na soko la ndani, bali kuiga mfano wa mataifa yaliyofanikiwa kujipenyeza  nchini mwetu na kuanzisha biashara zinazostawi. 

“Wametuonyesha kwamba inawezekana kufanya hivyo, ni wakati wetu sasa kuthubutu na kutumia fursa hii,tushirikiane pamoja, tuwe wabunifu, na kupanga mikakati pamoja ili kuhakikisha kwamba taasisi na mashirika ya umma yanajitegemea, yanachangia pato la taifa lakini  pia yanakuwa mojawapo kati ya mashirika makubwa duniani.”amesema.