December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TBA yajinasibu ujenzi majengo mbalimbali nchini

Na David John ,Geita

MBUNGE wa Geita Mjini Costantine Kanyasu ameupongeza Wakala wa Majengo hapa nchini (TBA) kwa kazi kubwa inayofanya ya kujenga majengo mbalimbali zikiwemo nyumba na ofisi za Serikali.

Akizungumza alipotembelea banda la TBA katika maonesho ya sita ya Madini yanayoendelea mkoani Geita katika halmashauri ya mji Geita kata ya Bombambili,Kanyasu amesema miongoni mwa kazi zinazofanywa na TBA zinaonekana hata katika mkoa wa Geita.

“Karibuni sana Geita, na nawapongeza kwa sababu nawaona kila Mwaka, kwa bahati nzuri Mkoa Geita mna kazi yenu nzuri, nimefika Chato, nimefika hospitali ya Mkoa kwa hiyo karibuni sana” amesema Mbunge Kanyasu

Awali Kaimu Meneja Mawasiliano na Masoko  TBA Fredrick Kalinga amesema,Serikali ya awamu ya sita iliona haja ya kuhuisha Sheria iliyoanzisha TBA kwa kuiboresha kupitia gazeti la Serikali  namba 595 la 25 Agosti 2023 ambayo inairuhusu TBA kushirikiana na Sekta binafsi kuendeleza miliki nchini kwa maana ya kujenga nyumba za kupangisha na kuuza kwa wananchi wote.

” Lakini pamoja na hayo tumekuja kuwaonyesha wananchi wa Mkoa huu wa Geita miradi ambayo Taasisi yao inatekeleza hasa maeneo haya ya Geita.”amesema na kuongeza kuwa

“Kuna miradi mbalimbali ambayo inatekelezwa na mingine tayari imekamilika kama hospitali ya rufaa ya Kanda ya Chato, hospitali ya rufaa ya Mkoa, majengo ya Ofisi ya Mkuu wa Mkuu wa Mkoa,

“Vile vile tunawaonyesha wananchi kwamba Serikali imehamia Dodoma na serikali imewekeza fedha nyingi kwenye Ujenzi wa Mji wa Serikali, hivyo tumekuwa tukiwaonyesha majengo  ambayo TBA inajenga katika Mji  wa Serikali”

Aidha amesema katika bajeti ya mwaka huu TBA inatarajia kuanza ujenzi wa jengo moja la ghorofa eneo la Msiitini.

” Pale tunategemea tutajenga jengo la gorofa ambalo chini litakuja eneo la Biashara, na juu litakuja eneo la Makazi.