January 13, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TATO waunga mkono Jeshi la Polisi Usalama kwa watalii

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Jeshi la Polisi kikosi cha Usalama Barabarani limesema litaendelea Kushirikiana na wadau wa Utalii ili kuweka mazingira bora ya usalama barabarani ambayo yatawashawishi watalii wa ndani na wale wanaotoka barani Afrika na Ulaya kuongezeka kwa wingi na kutembelea vivutio vilivyopo hapa nchini huku likipongeza wakala wa utalii Tanzania (TATO) kwa kufadhili safari yao katika hifadhi ya Taifa Tarangire.

Kauli hiyo imetolewa na afisa mnadhimu namba moja wa kikosi cha Usalama Barabarani Kamishna msaidizi wa Polisi ACP Pili Misungwi wakati walipo pata fursa ya kutembelea hifadhi ya Taifa ya Tarangire ambapo amebainisha kuwa kikosi hicho ambacho kina dhamana ya kusimamia usalama Barabarani kitaendelea kushirikisha wadau wa utalii ili kuweka uelewa wa Pamoja katika kusimamia masuala ya usalama wa Barabara kwa waongoza watalii hapa nchini.

ACP Pili ameongeza kuwa endapo madereva wa watalii watafuata sheria za usalama barabarani itasaidia kuleta imani kwa watalii wanaotumia vyombo vya moto kutembelea hifadhi mbalimbali zilipo hapa nchini huku akimshukuru Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Camillus Wambura kwa kuwapa fursa ya kutembelea hifadhi ya Taifa Tarangire.

Pia amemshukuru Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Utalii Tanzania (TATO) Bwana Sirili Akko kwa niaba ya bodi ya TATO kwa namna walivyo Fadhili safari yao katika hifadhi ya Taifa Tarangilie iliyopo kaskazini mwa Tanzania ambapo amebainisha kuwa hifadhi hiyo ni nzuri huku akiwaomba watanzania kutembelea hifadhi hiyo.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Utalii Tanzania (TATO) Bwana Sirili Akko amesema wataendelea kushikiana na Jeshi la Polisi kwa karibu huku akibainisha kuwa mtaji Mkubwa wa sekta hiyo ni usalama kwa watalii ambapo amebainisha kuwa mafunzo ya ukaguzi wa vyombo vya moto umekuja wakati sahihi kukiwa na wingi wa wageni wa ndani na nje ya Tanzania.

Bwana Sirili ametumia fursa hiyo kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara wa kutoa dira katika sekta ya utalii nchini ambayo ilichagizwa na filamu ya Tanzania The Royal Tour ambayo imesaidia kuongeza watalii wengi kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika na Ulaya.

Nae Mkuu wa Mkuu wa kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Arusha Mrakibu mwandamizi wa Polisi SSP Zauda Mohamed amesema kikosi hicho kimepata mafunzo ya viwango vyaa juu kulingana na mabadiliko ya teknolojia ya vyombo vya moto ambavyo vimekuwa vikiingia hapa nchini huku akiwaomba wadau wa utalii kutumia wataalam wa Jeshi hilo kufanya ukaguzi wa vyombo vyao ambavyo hubeba watalii.