Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Pwani
MPANGO wa serikali wa kunusuru kaya maskini kupitia mradi wake wa TASAF umemwezesha kijana Hassan Korola (17), mkazi wa Kitongoji cha Mwembe-Baraza, kata ya Janga katika halmashauri ya wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani kutimiza ndoto yake ya kusoma hadi Chuo Kikuu.
Akiongea na gazeti hili juzi kwenye ziara ya Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete katika kata hiyo, Hassan aliishukuru serikali kwa kuanzisha mpango huo kwa lengo la kuwezesha kaya zisizo na uwezo kuinuka kiuchumi.
Alisema hali duni ya maisha ya wazazi wake ilimkatisha tamaa na hakutarajia kusoma hadi hapo alipofikia, lakini kwa kudra za Mwenyezi Mungu ameweza kusoma kuanzia darasa la kwanza, sekondari na sasa Chuo Kikuu.
‘Nilikuwa natamani sana kufikia hatua hii kielimu, lakini kama sio maono mazuri ya serikali yetu ya CCM kujali wananchi wake wasio na kitu na kuanzisha mpango huo wa kunusuru kaya maskini kamwe ndoto yangu isingetimia,’ alisema.
Akishuhudia manufaa ya mfuko huo kwa niaba ya wanufaika wenzake mbele ya Naibu Waziri, Asia Mohamed (40) aliishukuru serikali ya awamu ya 6 kwa kuendeleza mradi huo na kuwezesha watoto wao kupata huduma za afya na elimu.
Alibainisha kuwa watoto wao wanapata mahitaji yao ya msingi ikiwemo chakula na wale wanaofanya vizuri zaidi darasani serikali haiwatupi, inawasiaidia hadi kufikia elimu ya juu.
Naibu Waziri Ridhiwani Kikwete aliwathibitishia kuwa serikali ina dhamira njema ya kuwaondolea umaskini wananchi wake ndiyo maana ikaanzisha mradi wa TASAF ili kuwezesha kata zote zisizo na uwezo na watoto wao.
Aliwataka wakazi wa Kitongoji cha Mwembe-Baraza na kata nzima ya Janga ambao wamenufaika na mpango huo kujitokeza kueleza kwa uwazi mafanikio waliyopata kupitia mpango huo ili serikali ijiridhishe na kuendelea kuwasaidia.
Aidha Naibu Waziri aliwataka kutumia vizuri fedha wanazopata ili ziwasaidie kubadili maisha yao ikiwemo kuanzisha miradi midogo kupitia fedha kidogo wanazopata ili kujiongezea kipato.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â