November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TASAF yawataka wana Nyasa kushirikiana kuwapata wanufaika wenye sifa

Na Netho Sichali,TimesMajira online,Nyasa

AFISA ufuatiliaji kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), makao makuu ya TASAF Salumu Mshana amewataka wananchi wa Wilaya ya Nyasa kushirikiana ili kuwapata wanufaika Mpango wa TASAF wenye sifa.

Ameyasema hayo hivi karibuni wakati akifanya ufuatiliaji wa uibuaji wa wanufaika wa mpango wa TASAF wakati wa mkutano ya hadhara uliyofanyika katika Kijiji cha Ukuli Kata ya Kingerikiti na Kijiji cha Luhangarasi Kata ya Luhangarasi Wilayani Nyasa akiwa anafuatilia jinsi zoezi la uibuaji linavyoendelea.

Afisa Ufuatiliaji wa TASAFkutoka makao makuu Dodoma Salum Mshana akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Ukuli,Kata ya Kingerikiti Wilayani Nyasa katika Mkutano wa Kijiji wa Kuteua wanufaika wa Mpango wa TASAF awamu ya pili Wilayani hapa.Picha na Ofisi ya DED Nyasa

Mshana amefafanua kuwa amefanya ufuatiliaji ili kuhamasisha jamii wenye sifa kujitokeza katika mpango wa kunusuru kaya maskini kipindi cha pili TASAF ili uweze kufanikiwa kwa kuwapata wanufaika waliokidhi vigezo.

Ameongeza kuwa tayari mafunzo yametolewa kwa viongozi wa wilaya na wawezeshaji ngazi ya jamii na katika vijiji 32 ambavyo awali havikuwa katika mpango huo.

Amewataka wananchi kuhudhuria katika mikutano inayoitishwa na viongozi wao na kuwaibua walengwa waliokidhi vigezo.

Ametoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu zoezi hilo ili liweze kukamilika kwa ufasaha.

Baadhi ya wanufaika wa TASAF wakimsikiliza mwezeshaji kutoka TASAF

“Nichukue fursa hii kuwaomba mshiriki kikamilifu kuwaibua wanufaika wanaostahili kwa kuwa mpango huu umeanza muda mrefu na umepitia changamoto mbalimbali sasa tunawataka wananchi wote mjitokeze kwa wingi katika mikutano ya kuwaibua wanufaika ili tuwapate wenye vigezo vya kitaifa na vigezo ambavyo wamepewa na wawezeshaji,” amesema.

Amewapongeza wananchi kwa kujitokeza kwa wingi katika mikutano na kuwaomba waendelee na mchakato mpaka ukamilike kwa kufuata utaratibu kwa kushirikiana na wawezeshaji ambao wamepewa mafunzo kwa ajili ya kutekeleza zoezi la utambuzi wa wanufaika hao.