Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Korogwe
MFUKO wa Maendeleo ya Jamii(TASAF) Halmashauri ya Mji Korogwe mkoani Tanga, kwa takribani miaka kumi umesaidia wanafunzi wengi kusoma shule za msingi, sekondari na kumaliza vyuo vikuu.
Pia TASAF imesaidia kutoa huduma za afya kwa watoto wadogo hadi wamekuwa, huku ikiwatoa wana kaya waliokuwa wanapata chakula kwa mlo mmoja kwa siku hadi mitatu na wengine wakiweza kufuga kuku, mbuzi, ng’ombe na kujenga nyumba kwa kuweza kuzungusha fedha za TASAF kwenye vikundi vya wekeza.
Hayo yamesemwa Julai 5, 2024 na Mratibu wa TASAF Halmashauri ya Mji Korogwe Rehema Letara wakati alipokuwa anatoa ufafanuzi kwa wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa Mtaa wa Kwamkole, Kata ya Mtonga, ambapo baadhi ya wanufaika hao wameondolewa kwenye mpango huo baada ya kujimudu kimaisha.
Ufafanuzi huo ulikwenda sambamba na malipo ya wanufaika kwa miezi ya Machi na Aprili, mwaka huu yaliyofanyika kwa siku mbili, ambapo Letara alisema Serikali iliamua kuwaongezea muda wa malipo hadi zaidi ya miaka tisa na baada ya kufanya tathmini walibaini baadhi ya wanufaika wanajiweza kwani sasa hivi angalau wana uwezo wa kula milo mitatu kwa siku.
“Wengi ni mashahidi na hata Mungu anaona Wakati mnaingia kwenye mpango miaka 10 kasoro wengi wetu tulikuwa hatuna uwezo wa kula milo mitatu lakini baada ya kuingia na kuwepo kwenye mpango kwa miaka kumi kasoro wengi wetu tuna kula milo mitatu kwa siku.
“Lakini pia mnafahamu kupitia TASAF, watoto wetu wameweza kusoma kwa ngazi tofauti kuanzia shule ya msingi sekondari na vyuo vikuu kwa kupewa mahitaji mbalimbali ikiwemo madaftari, kalamu, sare na viatu na wengine kusomeshwa hadi vyuo vikuu Lakini wengine wameweza kukuza biashara na mitaji yao na kuweza kununua kuku, mbuzi na hata ng’ombe,”amesema Letara.
Letara amesema ameomba waliofuzu ama kuondolewa kwenye mpango wasije wakamshika ‘uchawi’ kiongozi yeyote ngazi ya mtaa wala kata, kwani kuonekana kuwa wameimarika kiuchumi, ni baada ya kufanyika tathmini na baadhi yao kuonekana wana unafuu wa maisha.
“Msije mkataka kumlaumu kiongozi yeyote baada ya baadhi yenu kuonekana mmefuzu na kuondolewa kwenye mpango kama mnakumbuka kuna watu walikuja na simu kubwa (vishkwambi) na kuweza kuchukua taarifa ya kila mmoja wenu, ambapo katika maswali hayo, kuna ambao waliulizwa.
“Una shamba, nyumba unayoishi ina umeme, una friji, una kuku, mbuzi au ng’ombe. Je, maji unapata umbali gani kutoka hapo unapoishi. Na je, umeingiza maji kwenye nyumba unayoishi, na maswali mengine yanayofanana na hayo. Hivyo, baada ya kompyuta kuchakata, ndipo wakaonekana kuna waliofuzu, na kutolewa kwenye mpango” amesema Letara.
Letara amesema hata hivyo wanapokea malalamiko na kutakuwa na mtu wa kuchukua malalamiko hayo kila mtaa ili kuona kama kuna watu wametolewa kimakosa, hasa katika kujieleza na kuongeza kuwa jumla ya walengwa ambao walikuwa nao ni kaya 2,600, lakini kwa sasa waliotolewa baada ya kuhitimu ni kaya 1,707.
Naye Afisa Ufuatiliaji wa TASAF (TMO) kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, na Halmashauri ya Mji Korogwe Elizabeth Mwantyala kwa nyakati tofauti, aliwaeleza walengwa wa TASAF na wale waliotolewa kwenye mpango kuwa wataendelea kuwepo kwenye vikundi vya wekeza, kwani vikundi hivyo sio vya TASAF, bali vimeanzishwa na TASAF ili kuisaidia jamii kujiimarisha kiuchumi.
“Vikundi vya Wekeza vimeanzishwa ili kuwasaidia wananchi kujiimarisha kiuchumi, hivyo waliopo kwenye mpango, na wale waliotoka kwenye mpango, bado wanaweza kuendelea kuwemo kwenye vikundi hivyo. Vikundi hivyo sio vya TASAF wala Serikali, bali ni vya wananchi, hivyo mnatakiwa kuendelea kuvichangia, na viweze kuwasaidia kwenye shughuli zenu za kiuchumi na kijamii” amesema Mwantyala.
Naye mkazi wa Mtaa wa Kwamkole Mwanaisha Rajab ambaye alikuwa ananufaika na TASAF kupitia mlengwa Fatuma Rajabu Mohamed, ameishukuru Serikali kwa kuweza kuwahudumia kwa kuwapa fedha ambazo wameweza kujikimu kwa maisha yao kwa takribani miaka 10.
“Tunaishukuru sana Serikali yetu chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutulea karibu kipindi cha miaka 10 hadi leo hii ambayo tumeelezwa tumetolewa pamoja na hayo wawezeshaji wametupa elimu kwa kutueleza kila kitu kina mwanzo na kina mwisho kwa maana hiyo sisi tumefika mwisho hivyo hatuna buni kuishukuru Serikali.
“Na dada yangu (Fatuma) bado yupo kwenye kikundi na kwa vile bado ana changamoto ya mguu lakini nitaendelea kumpigania kuona bado anakuwepo kwenye kikundi na anafanya vizuri kwenye uwekezaji wa kikundi” amesema Rajabu.
More Stories
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato
Wambura asikitishwa na makundi CCM Nyakato