Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Kakonko
WAKAZI wilayani Kakonko Mkoani Kigoma wameelezea furaha yao na kupongeza juhudi kubwa zinazofanywa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha kiuchumi kupitia Mradi wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF).
Wakizungumza na gazeti hili hivi karibuni baadhi ya walengwa wa mpango huo wameeleza bayana kuwa maisha yao yamebadilika kwa kiasi kikubwa kupitia uwezeshwaji na mfuko huo tofauti na hali waliyokuwa miaka iliyopita.
Mkazi wa kijiji cha Kabigo kata ya Kiziguzigu wilayani humo Malieta Kayandabila (50) alieleza kuwa fedha anayopata kutokana na mfuko huo imemwezesha kufuga kuku na mbuzi na kuboresha nyumba yake ya kuishi.
‘Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia kwa kuendeleza mradi huu katika awamu yake ya uongozi, hakika umekuwa msaada mkubwa kwa kaya zote zisizo na uwezo ambazo zilitambuliwa na kuingizwa katika mpango huo’, alibainisha.
Mzee Mbwiliza Baheza (70) mkazi wa kijiji cha Kazilamihunda kata ya Kasanda, wilayani humo ambaye ni mnufaika wa mpango huo alisema familia yake sasa ina uhakika wa kupata milo 3 kwa siku kutokana na mradi wa genge alioanzisha.
Alibainisha kuwa wakazi wengi wilayani humo wana hali duni kimaisha, lakini ujio wa TASAF umekuwa mkombozi wao, kaya zote zilizotambuliwa na kuingizwa sasa zina uhakika wa kuishi kutokana na miradi midogo midogo waliyoanzisha ikiwemo kuanzisha vikundi vya kuweka na kukopeshana.
Akielezea mafanikio ya Mpango huo kwa wakazi wa wilaya hiyo, Afisa Mratibu wa Mpango huo Bi.Eusebia Barantanda alisema hadi kufikia Mei 2021vijiji vyote 44 vilivyoko wilayani humo ni wanufaika wa mpango huo.
Alibainisha kuwa tangu mpango huo kuanza kutekelezwa katika wilaya hiyo jumla ya walengwa 9,236 waliopo katika vijiji hivyo wanahudumiwa na mfuko huo na wengi wao wameanzisha miradi ya kiuchumi na kujiunga katika vikundi vidogo.
Eusebia alifafanua kuwa jumla ya vikundi 255 vya uzalishaji mali vimeundwa ili kusaidia wanufaika wa mpango huo kujiongezea kipato na kukidhi mahitaji yao ya msingi, vikundi hivyo vimepewa mafunzo ya uongozi na utunzaji kumbukumbu.
Aidha alisema baadhi ya vikundi hivyo vimepewa mafunzo ya uzalishaji na masoko ikiwemo masanduku ya kutunzia amana zao (kibubu), kalamu na kufuli kwa ajili ya utunzaji taarifa zao za kila siku.
Alieleza kuwa jumla ya kaya 5,542 kati ya 9,236 sawa na asilimia 60 ya kaya za walengwa wote zimefanikiwa kuanzisha biashara ndogo ndogo ikiwemo kufuga kuku, kondoo, nguruwe, sungura na bata hivyo kujiongezea kipato na kumudu gharama za maisha.
Aidha kaya 6,465 kati ya 9,236 sawa na asilimia 70 ya kaya wanufaika wote zimefanikiwa kuboresha makazi yao kwa kutoa nyasi na kuezeka nyumba kwa mabati huku kaya 8,035 sawa na asilimia 87 ya walengwa wote wana uhakika wa kula milo 3 kila siku.
Kuhusu suala la elimu na afya, Eusebia alisema kupitia mpango huo mahudhurio ya watoto shuleni yameongezeka hadi kufikia asilimia 100 na watoto wanaohudhuria kliniki wameongezeka hadi kufikia 2,735 sawa na asilimia 100.
Aliongeza kuwa utekelezaji mpango huo umeleta neema kubwa kwa wakazi wote wa wilaya hiyo waliotambuliwa na kuhawilishwa, hivyo kuonesha dhamira chanya ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupunguza umaskini kwa wananchi wake.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato