Na Allan Kitwe, TimesMajira Online, Kakonko
MPANGO wa Serikali wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) umeleta neema kwa wakazi Wilayani Kakonko Mkoani Kigoma baada ya kaya maskini zaidi ya 5,000 kuwezeshwa kupata Huduma za Bima ya Afya iliyoboreshwa kwa asilimia 100.
Hayo yamebainishwa na Mratibu wa TASAF Wilayani humo Eusebia Barantanda alipokuwa akiongea na mwandishi wa gazeti hili ofisini kwake hivi karibuni juu ya mafanikio ya Mpango huo katika miaka 3 ya Rais Samia.
Amesema kuwa katika kipindi cha miaka 3 ya utawala wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan jumla ya kaya 5,600 sawa na asilimia 62.94 ya kaya zote zinazonufaika na mpango huo zimejiunga na Mfuko wa Bima ya Afya iliyoboreshwa (iCHF).
Amebainisha kuwa wanafamilia wa kaya hizo sasa wanapata huduma zote za afya wakati wote hali ambayo imewaongezea matumaini ya kuendelea kuishi tofauti na huko nyuma.
Eusebia ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka 3 ya Rais Samia asilimia 60 ya kaya zote zinazonufaika na TASAF Wilayani humo zaidi ya kaya 8,000 zimeweza kujiongezea kipato na kumudu gharama za maisha kupitia fedha wanayopewa.
Ametaja baadhi ya miradi iliyoanzisha na kaya hizo kuwa ni pamoja na ufugaji kuku, mbuzi, kondoo, nguruwe, sungura, bata, miradi ya kilimo cha mbogamboga na mazao ya chakula na biashara.
Aidha amebainisha kuwa asilimia 95.5 ya kaya za wanufaika wote wa mpango huo zimefanikiwa kuboresha makazi yao ambapo baadhi wamejenga nyumba mpya za bati na wengine wameondoa nyasi na kuezeka kwa bati.
‘Tunamshukuru sana Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu mpango huu wa kunusuru kaya maskini uendelee kuwepo kwani umekuwa msaada mkubwa kwa kaya hizo na umeziwezesha kupata milo 3 kwa siku’, amesema.
Aidha mahudhurio ya watoto wanaotoka katika kaya hizo yameongezeka shuleni kutoka asilimia 85 hadi asilimia 99 na mahudhurio ya kliniki kwa watoto walio chini ya miaka 5 yameongezeka kutoka asilimia 75 hadi 100.
Baadhi ya wanufaika wa TASAF waliojiunga na Mfuko wa Bima ya Afya Wilayani humo, Rose Mutwe (50) na Yohana Luchugi (70) wamemshukuru sana Rais Samia kwa kuboresha mfuko huo na kuwawezesha kupata matibabu mazuri.
Mwisho.
More Stories
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari
Gridi za Tanzania, Kenya kuimarisha upatikanaji wa umeme
Mama Zainab:Watoto yatima ni jukumu la jamii yote