January 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TASAF kunufaisha 5,183 Buhigwe

Na Allan Vicent, TimesMajira Online Buhigwe

MIRADI 48 iliyobuniwa na wanufaika wa mpango wa serikali wa kunusuru kaya maskini (TASAF) Wilayani Buhigwe Mkoani Kigoma ili kukuza kipato chao inatarajiwa kunufaisha walengwa wapatao 5,183 kupitia ajira za muda mfupi.

Hayo yamebainishwa na Mratibu wa TASAF Wilayani humo Japhet Mombia alipokuwa akiongea na gazeti hili ambapo ameeleza kuwa jumla ya miradi 48 imebuniwa na kuanza kutekelezwa katika sekta ya ujenzi, misitu na maji.

Amefafanua miradi inayotekelezwa kuwa ni ya ujenzi wa barabara za jamii na vivuko vya waenda kwa miguu (miradi 38), uboreshaji vyanzo vya maji (miradi 8) na upandaji miti (miradi 2).

Mombia ameongeza kuwa utekelezaji miradi hiyo unafanywa na walengwa wa TASAF kwa ajira za muda mfupi ambapo kwa kila siku wanafanya kazi masaa 4 kwa ujira wa sh 3,000 ambazo hulipwa kupitia madirisha ya malipo yao.

‘Miradi hii imepokelewa kwa furaha kubwa kutokana na umuhimu wake kwa jamii, baadhi tayari imekamilika na mingine inaendelea kutekelezwa chini ya usimamizi wa Mhandisi wa halmashauri’, amesema.

‘Hadi kukamilika kwake zaidi ya sh mil 883.9 zinatarajiwa kulipwa na TASAF kwa walengwa wote kupitia dirisha la uhawilishaji wanufaika na jumla ya sh mil 120.5 zitatumika kununua vifaa vya kazi’, ameongeza.

Mratibu amebainisha kuwa miradi hiyo inasimamiwa na Kamati za Usimamizi za Vijiji (CMC) na inahusisha waengwa wote wenye uwezo wa kufanya kazi walio na umri kati ya miaka 18 hadi 65 ila sio wazee na wajawazito.

Amesisitiza kuwa miradi hiyo ilibuniwa na walengwa wenyewe kupitia mikutano mikuu ya vijiji vyao kati ya Juni1-5, 2021 chini ya uangalizi wa serikali za mitaa au vijiji vyao na kuanza kutekelezwa wilayani humo Novemba 2021.

Mombia ameishukuru serikali kwa kuwaletea kiasi cha sh mil 172 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya miradi hiyo na kuongeza kuwa zitakazobakia zitatumika kwenye miradi ya miundombinu ya afya au elimu kadri watakavyoelekezwa.

Walengwa wa TASAF katika kijiji cha Mnyegera kata ya Mnyegera, Wilayani Buhigwe Mkoani Kigoma wakishiriki kwenye mradi wa ujenzi wa barabara ya kijiji hicho ambao ni miongoni mwa miradi waliyobuni na kupewa fedha na TASAF kwa ajili ya utekelezaji wake. Picha na Allan Vicent Â