Na Ashura Jumapili,Bukoba,
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limetoa maboya zaidi ya 25 kwa wanafunzi wa shule za msingi za Rumuli Kashai, Nyamkazi wanaolazimika kutumia Ziwa kila siku kwenda shuleni kutoka visiwa vya Msira ikiwa ni juhudi za kuhakikisha wanakuwa salama.
Akizungumza wakati wa kufunga maonesho ya siku ya mabaharia duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Kagera Katibu Tawala wa Mkoa huo Profesa Faustine Kamuzora, ameipongeza TASAC na kusema kuwa pamoja na juhudi hizo Serikali imeendelea kuwekeza kwenye ujenzi wa meli ili kuhakikisha wakazi wa Kanda ya Ziwa wanakuwa na usafiri wa uhakika kwa njia ya maji.
“Niwapongeze kwa juhudi mnazozifanya za kuwafikia wananchi wanapata elimu sahihi na watoto wetu wanapata vifaa vitakavyowasaidia wanapotumia usafiri wa majini nawaomba pia tuendelee kutoa elimu zaidi ili kuendelea kuwanusu vifo vinavyotokea kutokuwa na vifaa sahihi vya majini’ amesema Prof. Kamuzora.
Prof. Kamuzora amewataka wananchi na wanafunzi hao kuvitunza vifaa hivyo ili viweze kudumu kwa muda mrefu kwani vimenunuliwa kwa kutumia fedha za Serikali huku akisisitiza Elimu zaidi kutolewa kwa wakazi wanasafiri kwenda visiwani kwani mkoa wa Kagera unavisiwa vinavyokaliwa na watu vipatavyo 39 hivyo Elimu ya usafiri kuhusu usalama wa maisha yao inahitajika.
Mwenyekiti wa bodi ya TASAC taifa Kapteni Musa Mandia, amesema Wakala pamoja na udhibiti unaendelea kusimamia viwango vya mabaharia ili kuhakikisha wanapata vyeti vyenye sifa za kuwaruhu kuajiriwa ndani na nje ya nchi.
Amesema kuwa Serikali imeendelea kuwekeza fedha kupitia Chuo cha Bahari Dar es Salaam ili kuhakikisha sekta inapata watalaam wa kutosha mkakati unaoenda sanjari na ujenzi wa meli katika maziwa nchini.
Naye Meneja wa Masoko na Elimu kwa Umma,Josephine Bujiku ambaye amemuwakilisha MKurugenzi Mkuu wa TASAC, amesema kupitia maonyesho hayo wamewafikia watu zaidi ya (3000 ) kwa kuwapa elimu ya usalama wa safari za makini ili kupunguza ajali zinazoweza kuepukika.
Siku ya mabaharia huadhimishwa kimataifa kila ifikapo 25 Juni kila mwaka ambapo kwa mwaka huu yamefanyika Kitaifa Mkoani Kagera na yamebeba kauli mbiu ya “Safari yako leo na kesho, toa ushirikiano’
Asimwe Jonathan ni mwanafunzi anayeishi kisiwa Cha Msira hulazimika kila siku kutumia usafiri wa maji kwaajili ya kwenda shuleni amesema maboya hayo yatawasaidia wakati wa kuvuka.
Jonathan, amesema wakati mwingine wanashindwa kuhudhuria masomo kutokana na changamoto za usafiri wakati wa mvua na upepo mkali hivyo hulazimika kukatisha masomo kwa baadhi ya siku.
“Tunaishukuru serikali kwa kutukumbuka na sisi kutugawia maboya kwaajili ya usalama wetu tunapokuwa tunaenda shule ili tuweze kusoma vizuri”amesema mwanafunzi huyo.
Amesema wanaiomba serikali kuwakea kivuko Cha kutoka kisiwa Cha Msira kuja Bukoba mjini ili kuweka mazingira salama ya usafiri kutoka huko kwa sababu kwa Sasa wanatumia mitumbwi ya kawaida ambayo wakati wa mvua na upepo ni changamoto kwao .
More Stories
CCM: TAMISEMI puuzeni makosa madogo madogo ,kukuza Demokrasia
Kamati ya Bunge yasema mradi wa umeme Rusumo,utazidi kuimarisha uhusiano mzuri wa Tanzania, Burundi, Rwanda
Leseni za Madini zaidi ya 50,000 zatolewa