November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TASAC yatoa gawio la bilioni 19.1 kwa serikali

Na Agnes Alcardo,TimesmajiraOnline,Dar

SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), limetoa gawio kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Shilingi bilioni 19.1, ikiwa ni sehemu ya uchangiaji katika mfuko wa hazina ya Taifa.

Gawio hilo, limetolewa Juni 11, 2024 Ikulu Jijini Dar es Salaam na kupokelewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, huku TASAC ikiwa kama moja ya taasisi za serikali zilizoshiriki katika utoaji wa gawio hilo.

Akiwasilisha hundi ya mfano wa kiasi hicho cha fedha, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mussa Mandia na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Nahson Sigalla.

Sigalla, ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita kwa kuchagiza Sekta ya Usafiri Majini na kupelekea matokeo ya ukusanyaji mzuri wa mapato.

“Tunaipongeza sana Serikali yetu ya awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia, kwa uongozi thabiti hasa katika sekta hii ya uchukuzi na kusababisha na sisi TASAC Kuchangia katika mfuko huu wa Hazina ya Taifa kwa kiasi cha shilingi bilioni 19.057 kama matokeo mazuri ya utekelezaji wa majukumu yetu,”amesema.

Akithibitisha utolewaji wa gawio hilo, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, alithibitisha kwamba TASAC imetoa gawio la shilingi bilioni 19.1 kwa mwaka unaoishia Juni 2024, huku akitoa shukrani za dhati kwa utendaji wao mzuri.

Aidha, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema hatakubali mtu yoyote amkwamishe kwenye azma yake ya kuleta mageuzi ya kiuchumi anayoendelea nayo na kwamba kila mmoja akafanye mageuzi ili kuongeza tija katika kukuza uchumi.

Amesema hataki kuona mtu yoyote anamkwamisha katika jambo hilo na kuwataka wakuu wa taasisi na viongozi wengine kuhakikisha wanaifanyia kazi falsafa hiyo na kuleta tija kwa Taifa na kuendelea kubakia katika uchumi wa kati.

“Hivi karibuni tumeingia tena kwenye kundi la uchumi wa kati kama ambavyo imeainishwa na wenzetu wa Benki ya Dunia, sasa ili uendelee kubakia katika kundi hilo ni lazima kuwe na mageuzi makubwa katika uchumi ili kuendelea kuaminika zaidi”, amesema Rais Dkt. Samia

Kuhusiana na mashirika yasiyofanya vizuri,Dkt.Samia amemtaka Msajili wa Hazina kuhakikisha anasimamia zoezi hilo na akishindwa basi yeye mwenyewe (Rais Samia) ataingilia kati na kuyafuta.

Amerudia tena agizo lake la kuhakikisha mifumo ya Serikali inasomana ifikapo mwezi Disemba mwaka huu bila kuwa na kisingizio chochote.