January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TASAC yajipanga kuhudumia wafanyabiashara, Diaspora Comoro


Na Mwandishi wetu

SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limejipanga kutatua changamoto za wadau wanaotumia usafiri wa njia ya maji wanaosafirisha mizigo baina ya Tanzania na Visiwa vya Comoros.
Akitoa salamu za Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Kaimu Meneja wa Usajili na Ukaguzi wa Meli, Mhandisi Said Kaheneko katika Kliniki ya Diaspora nchini Comoro iliyoandaliwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Comoro, amesema ushiriki wa TASAC utaleta matokeo chanya kwa kuwa wadau wa sekta ya usafiri majini watapata fursa ya kuelezea changangoto zao na Wawakilishi wa TASAC waliopo Comoro wataweza kukusanya na kutatua changamoto hizo ambazo zimewasilishwa.
“Timu ya watumishi wa TASAC kutoka Idara mbalimbali wanashiriki katika Kliniki na hii itakuwa ni fursa nzuri ya kuona namna ya kutatua changamoto za wadau wetu, kutoa elimu kuhusu masuala ya usalama wa vyombo, kutembelea bandari pamoja na kubadilishana Mawazo na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Majini ya hapa Comoro,” amesema Mhandisi Kaheneko.
Aidha amempongeza Balozi wa Tanzania nchini Comoro Saidi Yakubu kwa kuona umuhimu wa kuandaa Kliniki hii ambayo imejumuisha wadau mbalimbali wa Taasisi za Serikali na Binafsi kuweza kukutana na kutatua changamoto zinazowakabilia diaspora pamoja na kuangalia fursa zilizopo katika nchi ya Comoro.
Naye Balozi wa Tanzania nchini Comoro Saidi Yakubu amewashukuru Wakuu wa Taasisi wote walioruhusu maafisa wao kushiriki katika Kliniki ya Diaspora na kutoa rai kwa Diaspora kutumia siku hizo tatu kuweza kufika katika Kliniki ili kuweza kupata huduma.
“Shukrani za kipekee naomba nizipeleke kwa wakuu wote wa Taasisi zilizofika hapa, kwa kuitikia wito na kukubali kutoa huduma kwa watanzania wanaoishi Comoro. Naamini ujio huu utasaidia wao kupata huduma na changamoto zao kutatuliwa kwa wakati” amesema Balozi Yakubu.
Ubalozi wa Tanzania nchini Comoro umeaandaa Kliniki hii maalum kwa Diaspora katika viwanja vya Bunge, Moroni kuanzia Agosti 3 hadi 6, 2024 ambapo jumla ya Taasisi 17 zinashiriki na kutoa huduma katika Kliniki hiyo.