Zena Mohamed,TimesMajiraOnline,Dodoma
WAKALA ya barabara za vijini na mijini(TARURA) katika mwaka wa fedha 2023/24, inataraji kufanya matengezo ya jumla ya barabara zenye urefu wa km 21,057.06 ,huku km 427 zikijengwa kwa kiwango cha lami,na zingine km 8,775.62 zikijengwa kwa kiwango cha changarawe, pamoja na kujenga madaraja na makalavati 855 pamoja na mifereji ya mvua km 70.
Hayo yameelezwa jijini hapa leo,Agosti 24,2023 na Mtendaji Mkuu wa TARURA,Mhandisi Victor Seff wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu wa wakala hiuk na mwelekeo wake katika mwaka wa fedha 2023/24.
Amesema kuwa jumla ya shilingi bilioni 858.517 zimeidhinishwa kwa ajili ya ujenzi, ukarabati na matengenezo ya miundombinu ya barabara za Wilaya ambapo kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 710.31 ni fedha za ndani na shilingi bilioni 148.207 ni fedha za nje kupitia miradi ya RISE, TACTIC, Bonde la mto Msimbazi na Mradi wa Agri connect.
“Mojawapo ya kipaumbele cha TARURA ni kutumia malighafi zinazopatikana maeneo ya kazi ili kupata ufanisi wa gharama za ujenzi hadi Mwezi Machi, 2023 TARURA imejenga madaraja 163 ya mawe yenye thamani ya shilingi bilioni 8.7 ambapo gharama imepungua kwa zaidi ya asilimia 50,
“Madaraja hayo yamejengwa katika mikoa ya Kigoma 92, Singida 24, Tabora 5, Kilimanjaro 10, Mbeya 2, Arusha 6, Morogoro 2, Rukwa 3, Pwani 1, Ruvuma 3 na Iringa 15 pia tunaendelea kufanya majaribio ya teknolojia mbalimbali ili kutumia udongo uliopo eneo la kazi badala ya kusomba kutoka maeneo mengine ya mbali,Teknolojia hizo ni pamoja na ECOROADS, Ecozyme, na
GeoPolymer,”amesema Mha.Seff.
Akizungumzia utekelezaji katika mwaka wa fedha 2022/23 Mha.Seff amesema kuwa Wakala hiyo ilidhinishiwa jumla ya shilingi 838,158,970,993 kwa ajili ya ujenzi, ukarabati na matengenezo ya miundombinu ya barabara za Wilaya, kati ya fedha hizo, shilingi
776,628,938,748 ni fedha za ndani na shilingi 61,530,032,245.58 ni fedha za nje.
Ambapo utekelezaji wa kazi za ujenzi na matengenezo kwa Mwaka wa Fedha 2022/23 hadi kufikia mwezi Juni 2023, umefikia asilimia 85 ambapo jumla ya shilingi bilioni 743.405 zilipokelewa sawa na asilimia 89 ya bajeti iliyoidhinishwa. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 598.81 ni fedha za ndani na shilingi bilioni 144.593 ni fedha za nje.
“Kupitia fedha za ndani, jumla ya kilomita 22,523.51 zimefanyiwa matengenezo (utunzaji wa barabara), ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kilomita 249.74, ujenzi wa barabara kwa changarawe kilomita 9,761.01, ujenzi wa madaraja na makalavati 463 pamoja na ujenzi wa mifereji ya kuondoa maji barabarani kilomita 64.47,”amesema.
Hata hivyo Mha.Seff ametaja maeneo ya kipaumbele ya TARURA kuwa ni kuzitunza barabara zilizo katika hali nzuri na hali ya wastani kubaki katika hali hiyo ili kulinda uwekezaji ambao tayari umeshafanyika na kuondoa vikwazo kwenye mtandao wa barabara za Wilaya ili angalau ziweze kupitika misimu yote.
“Matumizi ya teknolojia na malighafi za ujenzi zinazopatikana eneo la kazi ikiwemo mawe katika ujenzi na matengenezo ya barabara kwa lengo la kuongeza ufanisi wa gharama, kupunguza muda wa utekelezaji na kutunza mazingira,
“Kupandisha hadhi barabara za udongo kuwa za Changarawe/Lami kwa kuzingatia vipaumbele vya kiuchumi na kijamii. Mipango ya muda mrefu ya Kitaifa na Kimataifa, ni pamoja na kupunguza msongamano wa magari katika majiji, manispaa na miji,”amesema Mha.Seff.
More Stories
Kiswaga:Magu imepokea bilioni 143, utekelezaji miradi
Zaidi ya milioni 600 kupeleka umeme Kisiwa cha Ijinga
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini