December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TARURA yafunga barabara zenye urefu wa Km 147 Mlele

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Mlele

WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilayani Mlele Mkoani Katavi wamefanikiwa kufungua mtandao wa barabara mpya zenye urefu wa zaidi ya km 147 katika kipindi cha miaka 3 ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.

Hayo yamebainishwa jana na Meneja wa TARURA Wilayani humo Mhandisi Paul Mabaya alipokuwa akiongea na mwandishi wa gazeti hili Ofisini kwake ambapo alieleza kuwa miaka 3 ya Rais Samia imekuwa na mafanikio makubwa sana.

Amebainisha kuwa mtandao huo ni wa barabara zinazounganisha vijiji na kata katika maeneo mbalimbali ambako hakukuwa na barabara rasmi zinazotambulika, hali iliyokuwa ikikwamisha shughuli za kiuchumi.

Amefafanua kuwa katika mtandao huo km 108.5 zimejengwa katika halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe na km 39.4 katika halmashauri ya Wilaya Mlele huku akibainisha kuwa mafanikio hayo yamechochewa na serikali kuwaongezea bajeti.

Mhandisi Mabaya amempongeza Rais wa awamu ya 6 Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwaongezea bajeti kutoka sh bil 1.3 walizokuwa wakipata huko nyuma hadi sh bil 5.2 kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ambazo zimewawezesha kufanya mambo makubwa.

Ametaja baadhi ya miradi ya kimkakati iliyotekelezwa kutokana na ongezeko la bajeti kwa taasisi hiyo kuwa ni ujenzi wa daraja kubwa la Msadya lenye urefu wa mita 60 ambalo linaunganisha kata za Chamalendi na Mwamapuli.

Mingine ni ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa km 11.6 katika Mji wa Inyonga, Kata ya Nsekwa na Kata ya Utende ambazo zimewezesha kuboreshwa mandhari ya maeneo hayo na kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji mazao.

‘Tunamshukuru sana Rais Samia kwa kuongeza bajeti ya TARURA, kwani imetuwezesha kupanua mtandao wa barabara za Wilaya nzima kuanzia Vijijini hadi Mijini na kuziwesha kupitika wakati wote’, ameeleza.

Amefafanua mtandao uliopo sasa kuwa ni barabara za lami km 13.77 (km 1.86 zipo Mpimbwe na km 11.55 Inyonga), changarawe km 175.49, udongo km 320.1, madaraja 2, makaravati ya kawaida 197 na ya boksi 10 na taa za barabarani 30.

Ametaja mikakati mingine ya Wakala huo kuwa ni kujenga km 5 za barabara za lami katika Mji wa Inyonga na km 10 nje ya Mji huo ikiwemo km 15 za lami katika eneo la Usevya, Kibaoni na Maji moto ndani ya Mji wa Mpimbwe.

Mingine ni kuendelea kuboresha barabara zinazounganisha vijiji na vijiji, kufungua barabara mpya, kuweka taa za barabarani na kujenga miundombinu ya maji (mitaro na kalavati) ili kuzuia uharibifu unaosababishwa na mvua.

Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Wilayani Mlele Mhandisi Paul Mabaya.
Daraja la Msadya lililojengwa na serikali ya awamu 6 kwa gharama ya zaidi ya sh bil 4 ili kumaliza kilio cha muda mrefu cha wakulima katika kata za Chamalendi na Mwamapuli katika halmashauri ya Mpimbwe kushindwa kusafirisha mazao yao kutoka shambani…