December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TARURA yaendelea kuboresha huduma za usafiri

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online. Newala

WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Halmashauri ya Mji wa Newala mkoani Mtwara, umeendelea kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji kwa kujenga miundombinu ya barabara na vivuko katika maeneo mbalimbali wilayani hapa.

Kwa mujibu Meneja wa TARURA Halmashauri ya Mji wa Newala Mhandisi Dickson Mkokota, ujenzi wa Barabara ya Kiduni–Makondeko-Mkunya kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita moja, utasaidia kurahisisha usafiri na kufikia kwa urahisi huduma za kijamii kwa sababu barabara hiyo ni njia inayoelekea moja kwa moja kwenye chanzo kikuu cha maji, yanayotumiwa na wananchi wote wa Newala.

“Ujenzi wa barabara hii, utagharimu zaidi ya sh. milioni 400, barabara itakuwa na mifereji ya kukusanya maji, makaravati na vivuko vidogo vinavyoingia kwenye mitaa hasa maeneo ya nyumba za ibada, ili kurahisisha usafiri kwa wananchi wa eneo hili waweze kusafirisha mazao yao kwa urahisi,” amesema.

Naye Shekhe Mpota, mkazi wa Newala ameishukuru serikali kwa ujenzi wa barabara hiyo itakayoleta unafuu mkubwa kwa wananchi, ambayo itasaidia kusafirisha mazao yao kwa urahisi ikiwemo korosho, mbaazi na ufuta.

“Tunaishukuru serikali kwa ujenzi wa barabara hii kwa sababu itatuondolea kero ya kusafirisha mazao yetu, hasa korosho kwa vile korosho zote za Newala mjini zinatoka mashambani ambako barabara hii, inaelekea na kuja huku mjini hivyo.

“Barabara hii ikikamilika itatusaidia sana wananchi kusafirisha mazao yetu na kufanya biashara kwa urahisi, pia ni njia rahisi ya kufika mpakani mwa Msumbiji kwa kupitia Mto Ruvuma,” amesema.

Mbali na utekelezaji wa mradi huo, alisema TARURA katika Halmashauri ya Mji wa Newala imekamilisha ujenzi wa Barabara ya Elimu kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita moja katika eneo la Nangwala.

Amesema pia imefanya matengenezo ya barabara za Newala mjini kwa kuchonga barabara kwenye makazi ya wananchi eneo la PCCB kilomita 16, ambazo tayari zimeshakamilika na imekamilisha ujenzi wa korongo eneo la Julia lenye urefu wa mita 150 na upana usiopungua mita tatu.

Kwa mujibu wa Meneja huyo, korongo hilo limesaidia kupunguza kero kwa wananchi kutokana na maji ya mvua, yaliyokuwa yanaathiri makazi ya watu na mashamba.

TARURA katika Halmashauri ya Mji wa Newala, unahudumia Mtandao wa Barabara wenye urefu wa kilomita 406 na jitihada za uboreshaji wa huduma za usafiri na usafirishaji, ili kuinua uchumi wa wananchi zinaendelea.