Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora
WAKALA wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) Mkoani Tabora wamemfukuza kazi Mkandarasi wa ujenzi wa barabara (Kampuni ya Batalion) kwa kushindwa kutekeleza kazi aliyopewa kwa wakati licha ya kupewa muda wa kutosha.
Uamuzi huo umechukuliwa juzi na Meneja wa TARURA Mkoani hapa, Mhandisi Edward Lemelo baada ya Mkandarasi huyo kushindwa kutimiza matakwa ya kimkataba licha ya kukumbushwa mara kadhaa.
Alisema Mkandarasi huyo ni miongoni mwa Wakandarasi 5 walioingia mikataba na Wakala huo kutekeleza miradi mbalimbali ya barabara katika wilaya zote 7 za Mkoa huo kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Alibainisha kuwa wamechukua hatua hiyo baada ya kutoridhishwa na utendaji wake katika mikataba 2 aliyosaini tangu mwezi Agosti mwaka jana ambapo walibaini mkataba 1 unakwenda vizuri lakini mwingine hauridhishi hata kidogo.
‘Serikali imetuletea fedha za kutosha ili kujenga barabara za wananchi katika wilaya zote mjini na vijijini ili zipitike wakati wote, hivyo kila mkandarasi anapaswa kuzingatia matakwa ya mkataba wake’, aisema.
Mhandisi Lemelo alibainisha kuwa Mkandarasi yeyote asiyetekeleza wajibu wake kwa wakati na kwa kiwango kinachotakiwa hatapewa kazi nyingine katika Mkoa huo, aliongeza kuwa wataendelea kuchukua hatua kama hizo kwa maslahi ya jamii.
Alibainisha kuwa katika mwaka wa fedha uliopita jumla ya wakandarasi 2 waliondolewa kwa kushindwa kutekeleza kazi yao kwa wakati na kwa mwaka huu wakandarasi 4 wameondolewa, na hawatapewa kazi tena ya barabara.
Mhandisi Lemelo alieleza kuwa jumla ya miradi 69 ya barabara yenye thamani ya zaidi ya sh bil 27 inatekelezwa katika wilaya zote za Mkoa huo katika mwaka wa fedha 2022/2023 na inatarajiwa kukamilika kabla ya Juni 30 mwaka huu.
Alisema kati ya miradi hiyo, 6 inatekelezwa wilaya ya Tabora, 10 Sikonge, 6 Nzega Vijijini, 9 Nzega Mjini, 10 Uyui, 9 Urambo, 10 Kaliua na 9 Igunga na barabara za lami zilizokwisha jengwa na Wakala huo hadi sasa ni km 100.7.
Alipongeza juhudi kubwa za serikali ya awamu ya 6 chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza bajeti ya matengenezo ya barabara kila mwaka ili kuboresha miundombinu ya barabara na mandhari ya wilaya zote za Mkoa huo.
Alisema katika mwaka wa fedha 2020/2021 Mkoa huo ulitengewa bajeti ya sh bil 8, mwaka uliofuataa 2021/2022 sh bil 29, mwaka huu 2022/2023 sh bi 29 na mwaka ujao wa fedha wameomba kiasi kingine kama hicho.
Mstahiki Meya wa manispaa ya Tabora alipongeza hatua iliyochukuliwa na Meneja wa TARURA Mkoa na kubainisha kuwa kama hatabadilika afutwe kabisa kwenye orodha ya wakandarasi wanaofanya kazi katika mkoa huo.
Alitoa wito kwa wakandarasi wote waliopewa kazi ya ujenzi wa miradi ya barabara katika Mkoa huo kuzingatia matakwa ya mikataba yao na kufanya kazi kwa weledi mkubwa ili waendelee kuaminiwa.
More Stories
Rc.Chalamila:Tunaendelea kuokoa majeruhi Kariakoo kwa ustadi mkubwa
Act Wazalendo yazindua ilani uchaguzi serikali za mitaa
Mhagama atoa somo kwa watendaji