January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania,India kushirikiana sekta ya Kilimo nchini

Na Mwandishi wetu, Timesmajira

MAMLAKA ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) imesema kuwa Tanzania inaweza kushirikiana na India katika kuendeleza kilimo hasa cha mchele kwani nchi hiyo imeendelea kwenye zao hilo ambalo wanauza hadi nchini Saudi Arabia.

Hayo yamebainishwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa TanTrade, Latifa Khamis wakati wa siku maalum ya India (India day) iliyofanyika katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea.Alisema nchi inaangalia namna ya kuingia makubaliano katika sekta hiyo ya kilimo na mafuta ya kula ya alizeti.

“Kama mnavyofahamu Tanzania tunaangalia jinsi gani tunaweza kuongeza thamani mafuta yetu ya kula haşa ya alzeti, wenzetu wa India wapo tayari ila wanataka tuwauzie ila Serikali inataka wao waje kuwekeza na kufanya uchakataji wote hapa.

“Kwahiyo sisi kama TanTrade jukumu letu ni kuhakikisha fursa hizo zinakuja na kupitia programu tunazofanya katika maonesho tunahakikisha fursa walizokuja nazo wafanyabiashara kutoka nje zinabaki hapa hapa nchini,” amesema

Amesema zaidi ya wafanyabiashara 40 kutoka India wamekuja nchini ambapo wametembelea maoneo ya viwanda nchini hivyo wanania na kwamba TanTrade itahakikisha inawaunganisha na watu wengine ili waweze kuwekeza Tanzania.

Kwa upande Mwenyekiti wa bodiKituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC),Binlith Mahenge amesema mpaka sasa wameweza kusajili miradi 730 kutoka nchini India ambayo inathamani ya Dola za Marekani zaidì ya Milioni 4000 na kwamba nchi hiyo ni wawekezaji wakubwa na wa nataka waendelee kuwekezà nchini.

Amesema Tanzania ni mahali pazuri pa uwekezaji kwani kuna usalama, amani lakini pia nchi imejiandaa kupokea wawekezaji kwa kuendelea kuboresha miundombinu ikiwemo ya umeme na reli ya kisasa ya SGR“Ushirikiano uliyopo kati ya Tanzania na India umejionesha katika miradi ya uwekezaji kwenye sekta ya elimu, afya na mradi mingine mbalimbali, TIC tutaendelea kuwahudumia wawekezaji vizuri kwani kwa sasa vikwazo vingi vya uwekezaji vimeondolewa.

Naye Kamishna wa Bima Bahayo Sakware amesema maonesho ya mwaka huu ya Sabasaba wamekuja na rai kwa wawekezaji kutoa India kuangalia namna ya kufanya uwekezaji kwenye maeneo ya bima mtawanyo ,bima za kilimo,afya kwasababu serikali yetu kupitia uongozi mahiri wa Rais Samia Suluhu Hassan tunategemea kuona watanzania wakiwa na afya njema kupitia bima ya Afya kwa wote.

“Tunahitaji makampuni mengi yenye uzoefu tofauti tofauti kuja kufanya biashara nchini na tunawakaribisha wote kwenye maonesho haya,tumetoa mada kuhusu fursa zilizopo kwenye kwenye sekta ya bima ,”amesema na kuongeza

“Tunahitaji uwekezaji kwenye bima ya mtawanyo,tunahitaji wawekezaji kwenye bima za afya ,tunahitaji wawekezaji kwenye mifumo ya kidigitali kuwezesha bima kupatikana kirahisi na wepesi,”amesema.