December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania yatiliana Saini mikataba mitatu na Umoja wa Ulaya kusaidia bajeti Kuu ya serikali

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ameshuhudia utiaji  Saini wa mikataba mitatu ya makubaliano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya kwa ajili ya kusaidia bajeti Kuu ya Serikali.

Mikataba hiyo mitatu  ni pamoja  na mradi  wa kukuza uchumi wa buluu ambao utasaidia kuleta mabadiliko ya tabia nchi ambao utagharimu kiasi Cha shilingi Milioni 279, Mradi wa  kuimarisha mifumo ya usimamizi wa Fedha za Serikali wenye thamani ya shilingi Milioni 167.9,pamoja na mradi wa kuimarisha mahusiano kati ya Tanzania na  nchi za ulaya  wenye thamani ya shilingi Milioni 15.2.

Akizungumza mara baada ya utiaji wa Saini hizo Dkt Samia amesema kwa miongo mingi, Jumuiya ya Umoja wa Ulaya imekuwa ni moja ya washirika  wa kimkakati katika kukuza maendeleo na kuboresha ustawi wa watu hapa nchini.

Aidha amesema,mpaka sasa, Tanzania imeshapokea takriban euro milioni 2.3 ambayo ni sawa na shilingi trilioni 5.9 kama msaada pamoja na fedha nyingi za mikopo ikiwa ni mikopo ya makubaliano na sio mikopo ya kibiashara kutoka Benki ya Uwekezaji ya Ulaya.

“Msaada huu umekuwa chombo cha kusaidia utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Kimkakati nchini Tanzania, miradi ya maendeleo nchini inatekelezwa kwa njia ya “CPA” ambayo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaichukulia kwa uzito mkubwa.”amesema Rais Dkt.Samia na kuongeza kuwa

“Kuboreka kwa ushirikiano wetu, kumesaidia kuongeza idadi ya watalii wanaotoka Jumuiya ya Umoja wa Ulaya kuja nchini ambapo kwa kwa mwaka 2022 idadi yao ni asilimia 31 ya wageni wote.”

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt.Mwigulu Nchemba amemshukuru Rais Samia kwa juhudi zake za kuiwezesha nchi kufanya kazi pamoja na Wadau wa Maendeleo katika mchakato wa kujiletea maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

“Tanzania na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya wana mahusiano ya zaidi ya miaka 48, katika miaka yote hiyo Umoja huo umeendelea kuwa karibu na Tanzania,lakini chini ya uongozi wako, tumeshuhudia mafanikio makubwa ikiwemo kusainiwa kwa Mpango mpya wa ushirikiano kwa Tanzania utakaodumu katika kipindi cha kuanzia mwaka 2021-2027.”amesema Dkt.Nchemba

Ameongeza kuwa “Katika uongozi wako, tumeimarisha uhusiano wetu na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya ambayo imekuwa mstari wa mbele kutusaidia katika miradi yetu ya maendeleo ikiwemo malipo ya Dola za Marekani milioni 12 kati ya Dola za Marekani milioni 67.87 kwa ajili ya kuboresha Viwanja vya Ndege vya Mikoa ikiwemo Kigoma, Tabora, Bukoba, Sumbawanga na Shinyanga.”

Awali  Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Natu Mwamba amesema Jumuiya ya Umoja wa Ulaya utatoa msaada wa euro milioni 53.7 sawa na shilingi bilioni 140 ili kuongeza nguvu katika bajeti ya Serikali kwa ajili ya kusaidia sekta saba za kimkakati.

Naye  Balozi wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya Nchini Tanzania anayemaliza muda wake Manfredo Fanti amesema kuna njia nyingi ya kuchangia maendeleo endelevu ya Tanzania ambapo njia moja wapo ni kutoa misaada inayoonekana moja kwa moja ikiwemo ya ujenzi wa shule, hospitali au barabara .

“Lakini leo tuko hapa tukiwa na njia tofauti ambayo tumekubaliana na Tanzania ambayo ni kuchangia fedha kwenye bajeti ya Serikali.”amesema Balozi Fanti

Kwa mujibu wa Balozi huyo ,Jumuiya ya Umoja wa Ulaya inajiandaa kushirikiana na Tanzania kuimarisha bandari ya Dar es Salaam ikiwa ndio lango la Afrika Mashariki kwenda ulimwenguni, pia kuimarisha na kuendeleza Miji ikiwemo utekelezaji wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Kasi katika Jiji la Dar es Salaam na Majiji mengine.