November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania yamkosha Rais wa Ujerumani


*Ni kwa utulivu wa demokrasia, utawala wa Sheria na utawala bora, asema ni sababu ya w’biashara kuja kuangalia fursa za uwekezaji

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

RAIS wa Shirikisho la Watu wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier, ameipongeza Tanzania chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuwa na utulivu kwenye masuala ya demokrasia, utawala wa sheria na utawala bora na kupelekea wafanyabishara wa Ujerumani wamevutiwa kuja Tanzania kuangalia fursa za uwekezaji.    

Rais Steinmeier ambaye alianza ziara yake ya siku tatu nchini jana, ametoa kauli hiyo Ikulu jijini Dar es Salaam wakati yeye na mwenyeji wake (Rais Samia), wakizungumza na waandishi wa habari.

Ameweka wazi kufurahishwa na moyo wa Rais Samia wa kuendelea kudumisha na kuendelea uhusiano huo na kuufanya uwe mzuri zaidi kwa ajili ya kesho yetu.

Amesema ujio wake nchini Tanzania umepokelewa vizuri sana na watu wa Ujerumani pamoja na Dar es Salaam na wana shauku, kwani wameona namna Rais Samia alivyoweza kujenga uchumi na katika suala zima la utawala wa sheria.

“Tumeona kazi kubwa ambayo imeishafanyika hata katika suala zima la kidemokrasia. Tumeona namna ambavyo umeweza kufanyakazi njema, tuna penda kuwahakikishia sisi watu wa Shirikisho la Ujerumani tunakwenda kusimama na ninyi kwa karibu,” amesema Steinmeier.

Amefafanua kwamba urafiki baina ya Tanzania na Ujerumani  utaendelea kuwepo kwa sababu ya uaminifu ambao nchi hizo mbili zinao.

Amesema ziara hiyo italeta matunda mazuri sana kwa upande wa mahusiano ya kiuchumi na katika sekta mbalimbali, hivyo ana uhakika wataweza kusimama na kutumia zaidi fursa zinazotokana na mahusiano baina ya nchi hizo mbili.

Amesema kwa mara mbili zote ambazo amekuja nchi ameona kuna kampui nyingi changa atakutana na wabunifu vijana katika suala zima la ushirika wa kiuchumi na kuweza kutoa mitaji zaidi ili kuwasaidia zaidi katika suala la uzoefu.

Amesema mazungumzo yao na Rais Samia walijadili juu ya uhusiano wa nchi hizo mbili na namna uhusiano huo utaendelea kuwa na nguvu zaidi na kuvuka hata mipaka ya kisiasa.

Rais Steinmeier, amesema ni muhimu kuwa na watu ambao ni wabobevu zaidi katika suala zima la uchumi wa kidigitali ili kuongeza ajira kwa kizazi kijacho.

Aidha, amesema waliongelea suala zima la watalii kutoka Ujerumani  ili kuendelea kudumisha ushirikiano baina ya nchi mbili na katika maeneo mengine, kielimu, kitamaduni.

Amesema nchi hizo mbili zina ushirikiano wa karibu kwa miaka mingi, wameona vyuo vingi vinatoa kozi mbalimbali ambazo zinawaleta karibu wanafunzi wa Tanzania na Ujerumani.

Aidha,  amesema walijadiliana namna ya kujenga mahusiano karibu katika maeneo mengine ya ushirikiano na maeneo mengine ya ushirikiano.

Amesema kongamano la wafanyabiashara wa Ujerumani na Tanzania litawafungua na kuweza kuona ni namna gani wanaweza kufanyakazi kwa karibu .

Amesema amefurahi kuwepo tena Tanzania, kwani hiyo sio mara ya kwanza. “Nimeshafika hapa mara mbili, lakini sasa hivi ndiyo nakuja mara ya kwanza kama Rais wa Shirikisho la Jamhuri ya Watu wa Ujerumani.”