Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba amesema Tanzania imejidhatiti kuhakikisha Jumuiya ya Afrika Mashariki inakuwa imara, yenye umoja na inayofikia malengo yake.
Akiongoza Mkutano wa faragha wa siku tatu wa Mawaziri wa Mambo ya Nje na Mawaziri wanaoshughulikia masuala ya Afrika Mashariki unaofanyika Zanzibar kuanzia tarehe 6-8 Julsi 2024, Mhe. Makamba amesema madhumuni ya mkutano huo ni kuwa na familia imara, kuiwezesha Jumuiya ya Afrika Mashariki kutekeleza majukumu yake vizuri na kuongeza kuwa Tanzania kama moja ya nchi waanzilishi wa Jumuiya hiyo imejidhatiti kuona jumuiya yenye umoja, imara na yenye kufanikisha mipango na malengo yake.
Amesema kufanyika kwa Mkutano huo kunatokana na maelekezo ya Wakuu wa Nchi na kuongeza kuwa ni matarajio ya Tanzania kuwa viongozi hao watazungumza kiungwana, kwauwazi kwa lengo la kuimarisha Jumuiya.
“Umoja ndio nguvu yetu, tumeona katika siku za nyuma tulipojaribu kuwa na umoja huu lakini ukavunjika, madhara ya kuvunjika kwa umoja ule bado tunayo na kwa hali hiyo hatupaswi kurudia tena makosa hayo,” alisema Mhe. Makamba.
Akizungumza katika kikao hicho Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Musalia Mudavadi ameipongeza Tanzania kwa kukubali kuwa mwenyeji wa mkutano huo na kuongeza kuwa ni wakati muafaka kwa nchi wanachama kuhakikisha wanatumia fursa mbalimbali ndani ya jumuiya kwa manufaa ya wananchi.
Naye Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Afrika Mashariki wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Rebecca Kadaga ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuwa mwenyeji wa mkutano huo na kupongeza juhudi za kuimarisha jumuiya ambazo zimeoneshwa kuchukuliwa na viongozi wakuu.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la EAC Mhe. Dend Alor Kuol amesema kufanyika kwa Mkutano huo ni jambo jema hasa ikizingatiwa kuwa unaangalia masuala ya amani, usalama na mtangamano wa jumuiya ikiwa ni hatua maridhawa katika kuifanya jumuiya kusonga mbele.
Mkutano huo wa faragha unajadili taarifa ya Mwenyekiti wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya; hali ya amani, usalama, siasa na uhusiano kati ya nchi wanachama; unatathmini na kujadili mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na masuala yanayokwamisha ufikiwaji wa malengo ya programu na miradi inayojiwekea.
Mkutano huo umeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 07 Mei, 2024.
Mawaziri kutoka nchi Nane Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki za Burundi, DRC, Kenya, Rwanda, Somalia, Sudan Kusini, Uganda, na Mwenyeji Tanzania wanahudhuria mkutano huo. Mkutano huo pia unahudhuriwa na Makatibu wakuu kutoka katika Wizara hizo na Wajumbe wa Sekretarieti ya EAC.
More Stories
Dkt.Tulia ashiriki ibada, asisitiza waumini kushiriki uchaguzi serikali za mitaa
Polisi yaonya vyama vya siasa
Mzumbe yaanika siri ya shahada udaktari wa heshima kwa Samia