
Na Mwandishi Wetu, Morogoro.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Balozi Baraka Luvanda, amekitaka Kituo cha Taifa cha Kufuatilia Kaboni (NCMC) kuongeza juhudi ili kuiwezesha Tanzania kushiriki kikamilifu katika masoko ya kimataifa ya biashara ya kaboni, lengo likiwa kuongeza mapato na kuimarisha uhifadhi wa mazingira nchini.
Akizungumza wakati wa ziara yake ya kwanza ya kikazi katika kituo hicho tangu kuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Luvanda amesema ni muhimu kuimarisha miradi ya kaboni inayohusisha sekta mbalimbali ili kuongeza fursa za kiuchumi na kuchochea maendeleo endelevu.
Ametaja sekta zenye mchango mkubwa katika biashara hiyo kuwa ni misitu, uchumi wa buluu na nishati mbadala, akieleza kuwa miradi katika maeneo hayo inaweza kusaidia kupunguza uzalishaji wa gesi joto huku ikiifanya Tanzania kunufaika na soko la kimataifa la kaboni.
Luvanda ameongeza kuwa biashara ya kaboni duniani inaendelea kukua kwa kasi, hivyo Tanzania ina nafasi kubwa ya kuvutia uwekezaji na kupata mapato ikiwa itaendelea kuwekeza katika uhifadhi wa mazingira na miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa NCMC, Kathryn Kigaraba, amesema kituo hicho kitaendelea kusimamia ufuatiliaji wa gesi joto na uratibu wa biashara ya kaboni nchini, akibainisha kuwa taasisi hiyo ilianzishwa chini ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura ya 191 ili kuratibu shughuli zote zinazohusiana na soko la kaboni Tanzania.

More Stories
DC Mbozi afuturisha wananchi, asisitiza mshikamano na Umoja.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali: Nina imani mubna utendaji kazi wa ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria
Wanawake wahimizwa kuchangamkia fursa za kiuchumi