January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania, Ujerumani kushirikiana kuboresha utamaduni

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online, DSM

Serikali ya Tanzania pamoja na Shirikisho la Ujerumani zimekubaliana kuongeza ushirikiano katika kuboresha masuala ya utamaduni na malikale ili kuendelea kuhifadhi urithi wa historia ya nchi kwa faida ya kizazi kilichopo na kijacho.

Ahadi hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Shirikisho la Ujerumani Mhe. Katja Keul wakati alipokutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Balozi Mulamula amesema kuwa Ujerumani imekuwa na msaada mkubwa katika maendeleo ya kijamii, kitamaduni, kielemu na kiuchumi. “Kwa sasa tunaadhimisha miaka 60 ya ushirikiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Ujerumani. ziara ya Mhe. Keul hapa nchini imelenga kuangala namna gani tunaweza kuongeza ushirikiano katika masuala ya utamaduni na malikale ambapo katika kutimiza hilo tayari mkataba wa ushirikiano wa kuendeleza makumbusho yetu ya taifa umesaini jana,” amesema Balozi Mulamula.

Nae Waziri Keul amesema kuwa Ujerumani na Tanzania zinaadhimisha miaka 60 ya ushirikiano na lengo kuu ni kuongeza ushirikiano katika masuala ya utamaduni na malikale kwa maslahi ya pande zote mbili.

“Katika kuhakikisha tunaongeza na kuboresha ushirikiano katika masuala ya utamaduni na malikale, tumesaini mkataba wa ushirikiano kati ya Makumbusho ya Taifa na Mfuko wa Utamaduni wa Ujerumani lengo kwa lengo la kuhakikisha malikale na uhifadhi wa historia zinalindwa na kusaidia jamii kisayansi, kielimu,kiutamaduni na kiuchumi,” amesema Mhe. Keul

Kwa mujibu wa Sera ya Malikale ya mwaka 2008, malikale hujumuisha rasilimali za urithi wa utamaduni zinazoshikika na zisizoshikika; zinazohamishika, na zisizohamishika, zilizo nchi kavu na majini ambazo zinadhihirisha mabadiliko ya kimaumbile, kifikra, zana, vyombo na mazingira aliyoishi na kutumia binadamu na zenye umri wa miaka mia moja (100). Malikale hizi zinajumuisha zana za mawe na chuma, vyombo vya usafiri, metali, miti na mifupa; visukuku vya binadamu, mimea na wanyama; michoro ya miambani; miji ya kihistoria, magofu ya majenzi.