Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesaini makubaliano na nchi ya Uganda yanayolenga kudhibiti magonjwa ya mifugo yanayovuka mpaka baina ya nchi hizo mbili.
Makubaliano hayo yamesainiwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega kwa upande wa Tanzania na Waziri wa Kilimo Mhe. Bright Rwamirama kutoka Uganda, tukio lililofanyika Septemba 07, 2023 kwenye Ofisi za Wizara ya mambo ya nje jijini Dar-es-salaam.
Akizungumza kabla ya kusaini Makubaliano hayo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema kuwa utafiti umeonesha uwepo wa magonjwa mbalimbali ya mifugo ni miongoni mwa sababu za kushuka kwa mchango wa sekta ya mifugo kwenye pato la Taifa.
“Ni lazima tufanye udhibiti wa pamoja na wenzetu wa Uganda ambao mifugo yao imekuwa ikiingiliana na ile iliyopo nchini, hivyo tumekubaliana kuwa na kalenda moja ya chanjo za kudhibiti magonjwa ya mifugo”Amesema Mhe. Ulega
Aidha Mhe. Ulega amebainisha kuwa hatua hiyo ni matokeo ya mazungumzo kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni ambao waliafikiana kuchukua hatua ya pamoja katika udhibiti wa magonjwa yanayovuka mpaka.
“Tumeona tuwe na mpango wa miaka mitano ambao ni kampeni maalum ya uchanjaji wa mifugo utakaolenga magonjwa 5 tuliyoamua kuyapa kipaumbele na katika hilo tumeweka azimio la kuhakikisha ndani ya kipindi hicho tuwe tumeyapiga vita na ikiwezekana tuwe tumeyatokomeza kabisa” Aliongeza Mhe. Ulega.
Kwa upande wake Waziri wa Kilimo wa Uganda Mhe. Bright Rwamirama amesema kuwa amefurahishwa na hatua hiyo ambapo ameweka wazi itawasaidia kudhibiti magonjwa ya mifugo nchini mwao ambayo mengi yametokana na tabia ya mifugo hiyo kutembea kutoka eneo moja kwenda jingine bila kujali mipaka iliyopo baina ya maeneo hayo.
Awali, akiwakaribisha viongozi hao, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe amesema kuwa makubaliano hayo ni huru na upande wowote utakaokusudia kujitoa utapaswa kutoa notisi ya kipindi kisichopungua miezi sita.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakani
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best