December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania na Korea Kusini zaingia makubaliano kuimarisha sekta ya Ardhi

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeingia makubaliano na Wizara ya Ardhi  Miundombinu na Usafirishaji ya Korea Kusini kwa ajili ya kuimarisha sekta ya ardhi.

Makubaliano hayo yametiwa saini jana na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi wa Tanzania  Dkt Angeline Mabula na yule wa  Ardhi, Miundombinu na Usafirishaji wa Korea Kusini Bw. Won Hee-ryong katika mji wa Seoul Korea Kusini  kipitia hati ya makubaliano (MOU) ya ushirikiano kwenye sekta ya ardhi na menejimenti ya taarifa za kijiografia.

Makubaliano ya nchi hizo mbili yanalenga kuweka mazingira rafiki kwa watanzania kupata utaalam na uzoefu kwenye nyanja za upimaji na ramani kupitia mipango/miradi ya mafunzo ya kuendeleza rasilimali watu kwa maendeleo endelevu ya sekta ya ardhi, ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa fursa zaidi kwa watanzania kupata mafunzo ya muda mrefu nchini Korea.

Pia kuimarisha ushikiano uliopo kati ya Wizara ya Ardhi ya Tanzania na ile ya Korea Kusini katika kukuza matumizi ya teknolojia za kisasa kwenye sekta ya ardhi ili kuboresha utoaji huduma katika fani zote za utawala wa ardhi na kutimiza azma ya Serikali ya kusajili ardhi yote nchini.

“Wizara inaona upo umuhimu wa kuwa na makubaliano rasmi ya kukuza na kuimashira ushirikiano wa nchi hizi mbili kupitia Wizara ya Ardhi na wenzetu wa Korea kupitia Hati ya Makubaliano ya ushirikiano katika sekta ya ardhi na menejimenti ya taarifa za kijiografia” alisema Dkt Angeline Mabula.

Mbali na utiaji saini makubaliano hayo Dkt Mabula akiwa nchini Korea Kusini atashiriki  mijadala kwenye maonesho ya maendeleo ya teknolojia ya taarifa za kijiografia – Smart Geospatial Expo 2022.

Maonesho hayo yamekuwa yakifanyika kila mwaka sambamba na mikutano ya majadiliano ya kuanzisha na kukuza ushirikiano kwenye sekta ya ardhi inayowakutanisha viongozi wa juu wa serikali na makampuni ya kimataifa yanayojihusisha na taarifa za kijiografia kwa ajili ya maendeleo na usimamizi wa sekta ya ardhi. 

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi wa Tanzania  Dkt Angeline Mabula (Kulia) na Waziri wa Ardhi, Miundombinu na Usafirishaji wa Korea Kusini Bw. Won Hee-ryong wakisaini hati ya makubaliano (MOU) ya ushirikiano kwenye sekta ya ardhi na menejimenti ya taarifa za kijiografia jijini Seoul Korea Kusini jana.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi wa Tanzania  Dkt Angeline Mabula (Kulia) na Waziri wa Ardhi, Miundombinu na Usafirishaji wa Korea Kusini Bw. Won Hee-ryong wakionesha hati ya makubaliano (MOU) ya ushirikiano kwenye sekta ya ardhi na menejimenti ya taarifa za kijiografia mara baada ya kusaini jijini Seoul Korea Kusini jana.