December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania na Indonesia kushirikiana sekta ya umeme, mafuta na Gesi

Na.Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Waziri wa Nishati, January Makamba amefanya ziara ya kikazi nchini Indonesia, lengo likiwa ni kuimarisha ushirikiano wa nchi hizo mbili katika sekta ya umeme, mafuta na gesi.

Ziara hiyo imefanyika tarehe 9 hadi 10 Februari, 2023 ambapo Waziri Makamba kwa nyakati tofauti alikutana na Waziri wa Nchi anayeratibu biashara zinazomilikiwa na Serikali Mhe. Luhut Pandiaitan, Waziri wa Nishati na Rasilimali za Madini Mhe. Arifin Tasrif, Mwenyekiti wa Jukwaa la Biashara na Viwanda, Bw. Suryo Sulisto, Rais wa Shirika la Umeme la Indonesia (PLN), Bw. Darmawan Prasodjo, Makamu wa Rais wa Kampuni ya Mafuta ya Taifa ya Indonesia – Pertamina, Bw. Salyadi Sapurta, na Rais wa Kampuni ya Mafuta na Gesi ya MEDCO, Bw. Hilmi Panigoro.

Kwa Upande wa Waziri Makamba, aliongozana na Balozi wa Tanzania nchini Indonesia Mhe. Macocha Tembele, Kamishna na Petroli na Gesi, Bw. Michael Mjinja, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la TPDC Dr. James Mataragio na maafisa kutoka TANESCO na PURA.

Waziri Makamba ameeleza kuwa Tanzania inaona haja ya kuimarisha ushirikiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Indonesia katika maeneo ambayo ni masuala ya Umeme, mafuta na gesi.

Kwenye umeme, “Tanzania inahitaji kuimarisha uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa Nishati ya Umeme kwa wananchi wake na hivyo Indonesia ni nchi ambayo imepiga hatua kubwa na kwa haraka katika kufanikiwa kuwafikishia wananchi wake huduma hiyo. Hatuna budi kujifunza kutoka kwenu.” – Waziri Makamba.

Hadi sasa Indonesia imeshafanikiwa kufikisha huduma ya Umeme kwa asilimia 99.9 ya wananchi wake licha ya nchi hiyo kuwa na visiwa zaidi ya 1000.

Kwa upande wa Mafuta na Gesi, Waziri Makamba aliupongeza uongozi wa kampuni ya Pertamina na kampuni yake tanzu ya Maurel and Prom inayofanya kazi Tanzania katika kitalu cha Mnazibay kwa kazi zote zinazoendelea. Pia, alimueleza mweyeji wake kuwa, kampuni hiyo inaweza kufanya vizuri zaidi kwenye uwekezaji wa kitalu hicho.

“Serikali inatambua kitalu hicho bado kina rasilimali ya gesi nyingi zaidi ardhini, lakini uwekezaji wake hauridhishi. Serikali ya Tanzania inategemea sana uzalishaji wa gesi kutoka Mnazibay, ni vema Pertamina ikaliangalia jambo hili kwa kina kwa kushrikiana na mbia wake TPDC.” – Waziri Makamba.

Baada ya Kikao hicho Viongozi hao wa nchi mbili walikubaliana mambo yafuatayo; kusaini makubaliano ya awali ya ushirikiano kati ya Wizara na Nishati ya Tanzania na Wizara ya Nishati na Rasilimali za Madini ya nchini Indonesia katika kuendeleza miradi ya jotoardhi, usafirishaji wa umeme, utafutaji wa mafuta na gesi asilia na mafunzo ya kuongeza uwezo kwa wataalamu.