December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania, Msumbiji kuwabana pumzi magaidi

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Stergomena Tax, ameshiriki Mkutano wa Tume ya pamoja ya Masuala ya Ulinzi kati ya Tanzania na Msumbiji, uliofanyika kwa siku nne kuanzia Septemba 11 hadi Septemba 14, 2023, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam.

Na Iddy Lugendo, Timesmajira Online DSM

WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Dk Stergomena Tax amesema Tanzania na Msumbiji kushirikiana katika suala zima la ulinzi na usalama ili waweze kutokomeza ugaidi ambao umekuwa tishio katika mipaka yao.

Dk Tax amesema uhusiano wa nchi hizo umejengwa kihistoria tangu wakati wa mapambano ya ukombozi, akisema tulipigana pamoja, kushinda pamoja na tunapaswa kubaki na umoja huo.

“Tuko tayari kufanya kazi kwakaribu na Msumbiji ili kuimarisha zaidi ushirikiano wetu wa ulinzi na usalama. Kwa pamoja, tunaweza kushinda changamoto tunazokabiliana nazo na kujenga mustakabali ulio salama na wenye mafanikio zaidi kwa mataifa yetu, eneo letu na watu wetu,” amesema Dk Tax.

Ameyasema hayo wakati akifungua Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Masuala ya Ulinzi na Usalama wa tano (JPCDS-5th) ulioanza siku nne zilizopita.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Stergomena Tax, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Mkutano wa Tume ya pamoja ya Masuala ya Ulinzi kati ya Tanzania na Msumbiji, uliofanyika kwa siku nne kuanzia Septemba 11 hadi Septemba 14, 2023, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo umekutanisha watendaji wa juu katika Idara mbalimbali za masuala ya ulinzi na usalama kutoka nchi hizo
huku Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ikiongeza miezi 12 ya utekelezaji wa misheni ya SADC ili kurejesha usalama Jimbo la Cabo Delgado huko kaskazini mwa Msumbiji.

Katika eneo hilo, maelfu ya watu wameuawa na wengine zaidi ya laki saba kukimbia makazi yao tangu mwaka 2017 kutokana na uasi.

Mkutano huo unaakisi ziara ya Rais Samia Septemba 27-29 mwaka jana Msumbiji iliyoendesha majadiliano ya yaiyowezesha kusainiwa kwa mkataba wa makubaliano ya amani na usalama.

“Kwa hiyo mkutano huu unatupa fursa nyingine ya kuendeleza ushirikiano wetu, hasa katika maeneo ya ushirikiano yaliyomo katika mkataba wa makubaliano, Pia kutathmini maendeleo ya utekelezaji wa kikao cha nne cha JPCDS kilichofanyika Septemba mwaka jana, Maputo, Msumbiji’ amesema Dk Tax.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Ndani wa Msumbiji, Pascoal Ronda amesema kuhusu changamoto za uasi, uhusiano wa nchi hizo umekuwa na manufaa ya kihistoria.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Msumbiji, Pascoal Ronda, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Mkutano wa Tume ya pamoja ya Masuala ya Ulinzi kati ya Tanzania na Msumbiji, uliofanyika kwa siku nne kuanzia Septemba 11 hadi Septemba 14, 2023, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam.

“Juni 15 mwaka huu ikiwa ni baada ya miaka mingi ya mazungumzo magumu, Rais wa Jamhuri ya Msumbiji pamoja na kiongozi wa chama cha Renamo alifunga kambi ya mwisho ya kijeshi ya vikosi vya kukabili Vuguvugu la kigaidi huko Vunduzi, Wilaya ya Gorongosa, Mkoa wa Sofala.”

“Hatua hii ya kihistoria inaashiria mwisho wa mchakato wa upokonyaji silaha, uondoaji na urejeshaji Silaha, uliofanyika
kutokana na juhudi za ndani na nje ya Msumbiji na jumuiya ya kimataifa ikiwa ni pamoja na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

“Hatua hiyo inatoa mwelekeo wa maridhiano na utulivu wa nchi huku tukiwa na changamoto kubwa ya kupambana na ugaidi katika Jimbo la Cabo Delgado, ambako ni mapambano ya bila kupumzika huku tukiendelea na ushirikiano wa pamoja na jirani na ndugu zetu Tanzania.”

Viongozi mbalimbali wakifuatilia Mkutano wa Tume ya pamoja ya Masuala ya Ulinzi kati ya Tanzania na Msumbiji, uliofanyika kwa siku nne kuanzia Septemba 11 hadi Septemba 14, 2023, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam.