January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania miongoni mwa nchi 30 Duniani zenye wagonjwa wengi wa TB

Na Heri Shaaban, TimesMajira Online

Tanzania ni miongoni mwa nchi 30 Duniani zenye wagonjwa wengi wa TB ambazo huchangia asilimia 87 ya Wagonjwa wote Duniani (Takwimu za shirika la Afya Duniani (WHO)wa Mwaka 2021) .

Hayo yalisemwa na Mratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Dkt.Mbarouk Seif, wakati wa mafunzo kuhusu huduma za Kifua Kikuu kwa waandishi wa habari wa Dar es Salaam.

Dkt,Mbarouk Seif ,alisema mwaka 2021 Tanzania ilikadiriwa kuwa na wagonjwa 132,000 waliougua Kifua Kikuu, ikiwa ni sawa na uwiano wa wagonjwa 208 kwa kila jamii ya watu 100,000. Wagonjwa 87,415(65%) waligunduliwa na kuwekwa kwenye matibabu mwaka 2021.

“Wagonjwa 44,585 (35%) hawakuweza kufikiwa na kuwekwa kwenye matibabu hivyo kuendelea kuwaambukiza watu wengine katika jamii, hivyo ni jukumu letu kuendelea kuwatafuta kwa kila hali na kuwaweka katika matibabu Ili kupunguza maambukizi ya kifua Kikuu katika Jamii’ zetu na kutokomeza ugonjwa huo nchini .
Kwa upande wa Jiji la Dar es Salaam takwimu zinaonesha wagonjwa 5414 waliweza kuibiliwa na kuwekwa kwenye tiba mwaka 2022 ambayo ni sawa na asilimia 102 ya lengo la uibuaji (5311).

Dkt .Mbarouk alisema vituo vyote vya huduma za afya nchini vinatoa huduma za TB na Ukoma kwa viwango tofauti kulingana na uwezo wa kituo .

Akielezea hali ya maambukizi kwa mikoa kwa MIAKA mitano iliyopita mikoa ya Dar es Salaam ,Manyara ,Tanga ,Dodoma na Mwanza imekuwa imeripotiwa kuwa na kiwango cha juu cha uibuaji wa wagonjwa wa TB, aidha mikoa ya Katavi ,Rukwa Songwe na Njombe imeripotiwa kuwa na kiwango kidogo cha uibuaji wa wagojwa wa TB.

Mratibu wa TB Tanzania STOP TB Partnership Muungano wa wadau wa kupambana na Kifua kikuu Tanzania Nelson Telekera, alisema madhimisho ya Kifua Kikuu yanatarajia kufanyika Mkoa wa Simiyu Mwaka huu Machi 24 Mgeni Rasmi Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa, na Kaulimbiu ya siku ya Kifua Kikuu mwaka huu 2023 “Kwa pamoja tunaweza kutokomeza Kifua Kikuu nchini Tanzania “.

Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri Jiji la Dar Es Salaam Dkt ,Reginard Mlay, alisema ukiwa na Afya njema utafanya kazi zako vizuri na Uchumi wa nchi utakuwa .

Dkt.Mlay alisema madhimisho yanafanyika kila Mwaka Ili kuweza kufikisha ujumbe kwa jamii kuanzia ngazi ya kaya, mitaa, Kata,Wilaya mpaka Mkoa dhumuni kupeana elimu Ili ujumbe ufike kwa jamii kwa ajili ya mapambano ya Kifua Kikuu .

Mjumbe wa Bodi ya Tanzania stop TB Partnership Agatha Mshanga, alieleza mada ya umuhimu wanahabari katika kudhibiti Kifua Kikuu nchini Tanzania, alisema wanahabari wana mchango mkubwa kwa jamii katika kutoa elimu kuhusiana na Kifua Kikuu .

Agatha Mshanga alisema waandishi wa habari wana wajibu wa kuandaa habari na Makala mbalimbali, kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na ugonjwa huo na dhana potofu juu ya ugonjwa huo wa Kifua Kikuu na kuelimisha kwamba ugonjwa wa Kifua Kikuu unatibika, kupona na pia unaweza kuzuilika .

Kaimu Mganga wa halmashauri ya Jiji Dkt ,Reginard Mlay akifungua mafunzo ya waandishi wa habari wa Dar es Salaam katika mafunzo ya. Ugonjwa wa Kifua Kikuu (Picha na Heri Shaaban. )
Mratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Dkt .Mabrouk Seif akitoa elimu Kwa waandishi wa habari wa Dar es Salaam kuhusu elimu kuhusiana na ugonjwa wa Kifua Kikuu (Picha na Heri Shaaban )
Waandishi wa habari wa Dar es Salaam wakiwa katika mafunzo ya ugonjwa wa kifua kikuu kwa ajili ya kupewa elimu kuhusiana na ugonjwa huo (Picha na Heri Shaaban )
Mratibu wa kifua Kikuu na Ukoma Wilaya ya Ilala Mnazi Mmoja Dkt.Linda Mtasa akizungumza na waandishi wa habari wa Dar es Salaam waliokuwa wakipewa elimu kuhusiana na ugonjwa wa Kifua Kikuu Machi 14/2023 (Picha na Heri Shaaban )